Taasisi ya chakula na lishe Tanzania (TFNC) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) wamesaini mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa mwaka wa fedha 2021/2022 wenye thamani ya Shilingi milioni 575.7 sawa na USD 257,9.

Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa mkataba huo leo Agosti 19, 2021 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Germana Leyna amesema kuwa TFNC na WFP wamekuwa na ushirikiano wa muda mrefu tangu mwaka 2000.

“Kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2020/2021 WFP walitufadhili kufanya utafiti wa utengenezaji wa vyakula vya nyongeza kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi 59. Utafiti huu umefikia hatua nzuri ambapo tumeweza kutengeneza sampuli tano na katika hizo, sampuli mbili zimekubalika na kufanyiwa tathimini,” Amesema Mkurugenzi Dkt German.

Dkt. Leyna amebainisha maeneo makuu manne ya vipaumbele ambao wameingia nayo mkataba na WFP kuwa ni kusaidia masuala ya kisera, uratibu na usimamizi wa miradi, pamoja na eneo la tatu ni kuijengea uwezo Taasisi pamoja na wadau wa lishe nchini na kusaidia katika kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya chakula na lishe.

Katika hatua nyingine Dkt. Leyna amemuongoza Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania Sarah Godon-Gibson kutembelea maabara za TFNC kukagua baadhi ya mashine ikiwemo mashine ya kuchakata aina ya virutubish vilivyomo kwenye chakula (NIR) iliyonunuliwa na WFP kwa gharama ya shilingi milioni 67.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula nchini Tanzania Bi. Sarah Gordon-Gibson (aliyevaa koti jeupe) akielekezwa namna ya kuangalia mchanganyiko uliotumika kutengenezea chakula cha nyongeza kupitia teknolojia ya QR Code wakati alipotembelea maabara za TFNC zilizopo Mikocheni jijini Dar es salaam.
Wataalamu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) wakishuhudia zoezi la utiaji saini wa mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kati ya TFNC na WFP
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Germana Leyna (wa kwanza kushoto) na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula nchini Tanzania Bi. Sarah Gordon-Gibson wakionesha mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa mwaka wa fedha 2021/2022 mara baada ya kuusaini

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Augusti 20, 2021
Bashungwa asisitiza wadau kushiriki kwenye marekebisho kanuni za utangazaji