Uganda imekuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kufanya tamasha kubwa la kuwatafuta wawakilishi wa vijana wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) nchini humo kupitia shindano lenye muonekano sawa na yale ya kuwasaka warembo na watanashati.

Tamasha hilo la kumsaka mrembo na mtanashati wa VVU lilifanyika hivi karibuni jijini Kampala ambapo washiriki 150 waishio na maambukizi walijitokeza na kuchuana vikali jukwaani.

Mashindano hayo yalikamilika kwa kuwapata washindi ambao ni mrimbwende, Tryphena Natukunda na mtanashati Henry Kirabira (pichani).

Akizungumzia mashindano hayo, Mkurugenzi wa taasisi ya Uganda Network of Young People Living with HIV&AIDS, (UNYPA) ambao ndio waratibu wa tamasha hilo, Jacquelyne Alesi alisema wao hawaangalii urembo au uzuri wa mshiriki bali wanachoangalia ni uzuri wa ndani wa mshiriki atakayekuwa balozi mzuri wa kupambana na unyanyapaa.

“Hatuangalii labda una umbo zuri au ana mavazi mazuri, ama uzuri wa sura yako,” alisema Alesi.

“Sisi tunamtafuta mtu atakayetusaidia kupambana na unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na maambukizi ya VVU,” aliongeza.

Diamond amkaribisha Ali Kiba WCB
Diamond aeleza sababu za kuipeleka WCB kwa Kikwete