Rapa Wakazi amewataka mashabiki wake kukaa mkao wa kupokea mzigo wa muziki mzuri kutoka kwenye Album yake mpya aliyoibatiza jina la ‘Kisimani’.

Wakazi amesema kuwa album hiyo ambayo imefanywa nchini kwa ushirikiano wa watayarishaji zaidi ya wanne imekamilika kwa asilimia 95 ikisubiri sauti ya mrembo mmoja tu wa Bongo Flava kuikamilisha kwa asilimia zote na kuipakua.

Akifunguka katika Ladha 3600 ya E-FM, Wakazi amesema kuwa ingawa amekuwa akitoa kanda mseto (mix tapes) kadhaa, kwake ni hatua kubwa kuona anatoa album.

“Inanipa excitement kwa sababu I have been waiting for long time. Nimekuwa nikitoa mixtape kama 5 na EP moja lakini kuiita hii kama album rasmi ni kitu kikubwa sana na nakithamini sana kwangu,” alisema. “So I can’t wait kwa ajili ya hii hapa kuweza kuwafikia mashabiki,” aliongeza.

Rapa huyo alisema kuwa katika album hiyo amewashirikisha wasanii ambao anaamini wataweza kufikisha kitu kizuri kwa mashabiki wake bila kujali majina yao.

Akizungumzia soko la album nchini, Wakazi amesema kuwa hana wasiwasi kwakuwa kuna wigo mpana zaidi hivi sasa ambapo biashara ya album inaweza kufanywa hata kwa njia ya mitandao.

“Unajua mtu anaposema kuwa soko sio zuri wakati hajapeleka bidhaa sijui ana maanisha nini. Kwa sababu siku hizi muziki umebadilika, soko ni watu ni suala tu la kuwashawishi mashabiki wako kununua kazi. Na jinsi ya kuinunua sio tu kwa kuipeleka kwenye duka mtaani, siku hizi kuna online platform,” alisema.

Wakazi aka Swag Bovu alianza kujipatia mashabiki wengi ndani ya bara la Afrika baada ya kufanya show bora kwenye jukwaa la Big Brother Afrika miaka mitatu iliyopita.

Majaliwa Asisitizia Suala la Maji Safi na Salama Afrika
Zinedine Zidane Afunguka Kuhusu Paul Pogba