Jumla ya kiasi cha Dola milioni 400, zinahitajika kwa haraka ili kuweza kusaidia kutoa huduma za msingi za mahitaji ya kibinadamu nchini Sudan Kusini.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa Habari jijini New York Marekani hii leo Julai 6, 2022 kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko nchini Sudan Kusini yanakabiliwa na uhaba wa fedha unaosababisha shughuli za misaada kusitishwa, kupunguzwa na uwezekano wa kukomeshwa kabisa.

Dujarric amesema, Mratibu wa misaada ya kibadamu wa Sudan Kusini, Sara Nyanti amemueleza hali ya kibinadamu nchini humo ni mbaya zaidi kuwahi kutokea tangu taifa hilo kuanza kuwekwa kwa kumbukumbu.

“Takriban watu milioni 8.9 ambao ni zaidi ya theluthi mbili ya idadi ya watu wa taifa hilo wanakadiriwa kuhitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi kwa mwaka huu 2022” amesema Nyati.

Aidha, amefafanua kuwa kuwa Umoja wa Mataifa na washirika wake wanahitaji dola bilioni 1.7 kusaidia watu milioni 6.8, lakini mpango wa msaada wa kibinadamu umefadhiliwa kwa asilimia 27 pekee.

“Takriban vituo 220 vya kutolea huduma ya msingi ya afya na hospital tisa za serikali zipo hatarini kusitisha kutoa huduma mwezi ujao wa Agosti hali hii ikimaanisha Watoto, wanawake na wanaume milioni 2.5 ambao tayari wapo katika hali mbaya kiafya hawataweza kupata huduma za afya wanazohitaji.” Ameeleza Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa

Bila kupatikana kwa ufadhili wa haraka, takriban watu milioni 1.9 watakuwa hawana maji safi, huduma za usafi, chakula na mazingira duni.

Sierra Leone (SLFA) yaanza uchunguzi upangaji matokeo
Ligi ya Mabingwa Afrika Mashariki kuunguruma Arusha