Bunge la Kumi na Moja linaendelea kushika kasi yake huku kashfa mbalimbali za ufisadi zikianza kutajwa katika mikutano inayoendelea.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amefikisha bungeni sakata la ufisadi wa zaidi ya shilingi trilioni 6.8 uliotokana na mkopo wa serikali kupitia Benki ya Stanbic yenye tawi lake nchini,  akiitaka serikali kueleza hatua iliyochukua dhidi ya watumishi waliohusika na sakata hilo kwa kupokea hongo ili kuongeza kiwango cha riba ya mkopo huo.

Kadhalika, Mbunge huyo aliyekuwa akiuliza swali la nyongeza, alisema, “Serikali haioni kwamba umefika wakati CAG aweze kufanya ukaguzi maalum wa mikopo yote ya kibiashara ambayo serikali imechukua katika kipindi hicho ili kuweza kujua kama pia kulikuwa kuna aina za rushwa za namna hiyo ambazo zimekuwa zinafanyika.”

Zitto alitaka kufahamu kama kuna nia ya Serikali kuifungulia kesi Benki hiyo ya Uingereza iliyotoa hongo kwa watumishi wa Tanzania ili waweze kufanikisha wizi huo.

Akijibu hoja za mbunge huyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alieleza kuwa CAG anao wajibu kikatiba kufanya uchunguzi huo ili kujiridhisha kuhusu utaratibu wa kutoa mikopo kupitia makampuni hayo na kama yana harufu za wizi na ufisadi.

Aidha, Masaju alimtaka Zitto kushirikiana na vyombo husika ikiwa ni pamoja na ofisi yake (Mwanasheria Mkuu) na kuwasilisha ushahidi utakaosaidia katika hatua stahiki ikiwa ni pamoja kufungua shauri mahakamani.

Bungeni: Mbunge ataka serikali Ihalalishe Bangi, Mirungi.. atoa utetezi wake
Uchaguzi Marekani: Ted Cruz amshinda Donald Trump Mchujo wa jimbo la Lowa