Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Watanzania wana kila sababu ya kulinda utamaduni na utu wao na katu wasiudhalilishe dhidi ya utamaduni wa kigeni.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 29 Februari 2024 wakati akimwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa mwaka wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa Mfuko huo.

Amesema, “kupitia kazi za sanaa lazima tuoneshe kuupenda utamaduni wetu na kuuishi na tunataka utamaduni huo uende mpaka nje ya mipaka ya nchi, kwani Taifa lisilo na utamaduni ni Taifa mfu hivyo tuuenzi utamaduni wetu ambao ni mzuri.”

Dkt. Biteko amewasifu wasanii nchini kwa kukataa kupuuza utamaduni wa Taifa na kuamua kwa pamoja kuupa heshima utamaduni huo kupitia kazi zao za sanaa.

Amesema kuwa, wasanii wanao wajibu mkubwa wa kulifanya Taifa kuwa hai, kuliondoa kwenye wimbi la kupotea duniani na kuwafanya watanzania waone lugha yao, tamaduni zao na desturi za Tanzania zinapaswa kuheshimiwa na kila mtu.

Ameongeza kuwa, kwa miaka mingi kazi ya Sanaa ilikuwa ni kuelimisha na kuburudisha lakini sasa imepanuka na imekuwa ni nyenzo ya kutengeneza ajira na ndio maana Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua kuufufua mfuko huo ambao ulianzishwa mwaka 1992 na ambao ulikuwa ukisuasua lakini sasa umeimarika.

Amesema pamoja na ukweli kwamba Sekta ya Utamaduni na Sanaa inaongoza kwa ukuaji kati ya sekta zote nchini ikikua kwa asilimia 19 lakini bado mchango wake kwa pato la Taifa ni duni kwani inachangia asilimia 0.3 na hii ikimaanisha kuwa Sekta inakua lakini haichangii zaidi.

Ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuweka mazingira mazuri kwa wasanii ili kukuza sekta ya Utamaduni na Sanaa sambamba na ukuaji wa uchumi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewataka Wasanii kutumia kazi zao za Sanaa kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu ili wananchi hao waweze kujitokeza kwa wingi na kuchagua viongozi wanaopenda maendeleo na kuunganisha wananchi.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na upendo wake kwa Wasanii nchini ndio maana ameufufua mfuko huo na kuweka fedha ambazo zinawasaidia wasanii katika kuanzisha, kuboressha na kupanua shughuli zao za Sanaa.

Amesema , pamoja na faida za Mfuko bado kuna changamoto mbalimbali kama vile wakopaji kutorejesha mikopo kwa wakati na mfuko kuwa na chanzo kidogo cha fedha ambapo Wizara inachukua hatua mbalimbali kushughulikia changamoto hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Stephen Byabato, Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma.

 

Waziri Mkuu wa Ethiopia awasili Nchini kwa ziara ya Kitaifa
Wataalam wabobezi China, Tanzania wajadili maboresho Kiuchumi