Kiungo mkabaji wa klabu ya Dinamo Zagreb, Arijan Ademi anasubiri adhabu ya kufungiwa itakayotolewa na shirikisho la soka barani Ulaya, baada ya vipimo alivyofanyiwa kubaini alikua ametumia dawa za kusisimua misuli.

Ademi, alifanyiwa vipimo mara baada ya mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, ambapo Dinamo Zagreb, walifanikiwa kushinda mabao mawili kwa moja dhidi ya Arsenal mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na uongozi wa Dinamo Zagreb, usiku wa kuamkia hii leo kupitia tovuti ya klabu hiyo ya nchini Croatia, zimeeleza kwamba, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 hatochukulia hatua zozote za kinidhamu klabuni hapo zaidi ya kusubiri maamuzi kutoka UEFA.

Katika mchezo dhidi ya Arsenal, Ademi, alionekana kucheza bila kuchoka hali ambayo ilikua tofauti na wachezaji wengine wa timu zote mbili, na ndipo jopo la watu wanaopima afya za wachezaji walipomshtukia na kwenda kumfanyia vipimo.

Hata hivyo maamuzi ya UEFA dhidi ya kiungo huyo, hayatoathiri matokeo ya mchezo husika, na badala yake itaendelea kutambulika Arsenal walipoteza kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.

Mgombea Ubunge Wa Chadema Anusurika Katika Ajali Ya Gari
Kimenuka Kambi Ya Super Eangles