Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Simba SC, watalazimika kwenda Benin kwa ajili ya mchezo wa mzunguuko wa pili hatua ya Makundi dhidi ya ASEC Mimosas.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ Simba SC italazimika kwenda Benin badala ya Ivory Coast ambako ndio nyumbani kwa ASEC Mimosas, kutokana na changamoto ya Uwanja.

Taarifa ya ‘CAF’ inaeleza kuwa, ASEC Mimosas itatumia Uwanja wa Benin, kufuatia Uwanja wao wa Robert Champroux kushindwa kukidhi matakwa ya Shirikisho hilo lenye dhamana na Soka la Afrika.

Viwanja vingine vya Soka nchini Ivory Coast vinaendelea kufanyiwa maboresho, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Fainali za Afrika za 2023 ‘AFCON 2023’ zitakazounguruma nchini humo.

Katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Hatua ya Makundi, Simba SC itaanzia nyumbani Februari 13 kwa kuikabili ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Baada ya hapo Simba SC itasafiri kwenda ugenini wakiifuata Union Sportive Gendarmerie Nationale (USGN) ya Niger katika mchezo wa pili wa hatua ya Makundi kisha itacheza dhidi ya RS Berkane ya Morocco.

Uchaguzi Kenya 2022: Kalonzo, Odinga kuungana, Ruto apotea
Ligi Kuu Tanzania Bara yapanda viwango Duniani, Afrika