Timu za vijana za Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC chini ya umri wa miaka 11 na 13, zinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kesho Alhamisi alfajiri kwenda kushiriki michuano ya vijana ya Chipkizi Cup inayotarajia kufanyika mkoani Arusha kuanzia Desemba 15 hadi 17 mwaka huu.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo mpya za Azam FC kushiriki michuano ya nje, awali zilianza kushiriki michuano ya Ligi ya Vijana ya Azam U-13 iliyomalizika Julai mwaka huu.

Michuano hiyo inayohusisha timu mbalimbali za vijana Afrika Mashariki, imeandaliwa na kituo cha kukuza vipaji cha mkoani humo, Future Stars Academy, ambayo imeialika Azam FC, iliyoamua kupeleka timu hizo mbili zinazofundishwa na Mwingereza Tom Legg.

Utaratibu wa michuano hiyo kwa timu za chini ya umri wa miaka 11 (U-11) zitacheza 7v7, mechi zao zikiwa za vipindi viwili kila kipindi kikiwa na dakika 15 huku kwa wale wa U-13 wakicheza 9 kwa 9, kila kipindi kikiwa na dakika 20.

Azam U-11 itaanza kufungua dimba keshokutwa Ijumaa kwa kukipiga na Lidi Ndogo D saa 7.15 mchana kabla ya kucheza na Moi Edu Cent B saa 10.35 jioni.

Ikivuka kwa kupata matokeo mazuri kwenye mechi hizo, Azam U-11 itaingia moja kwa moja hatua ya nusu fainali kabla ya kutinga fainali endapo itapenya katika hatua hiyo.

Aidha, nayo Azam U-13, itafungua dimba Jumamosi hii kwa kukipiga na wenyeji Future Stars saa 7.15 mchana, kabla ya saa 11.10 jioni kumenyana na Elite Soccer Academy, ikipita hapo itaingia nusu fainali na hatimaye fainali itakayofanyika Jumapili hii.

Tanzania yatofautiana na Trump
Askari afariki dunia, atumbuliwa risasi ya kichwa