Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 umepitishwa rasmi leo Novemba 5, 2016 Bungeni mjini Dodoma katika mkutano ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Andrew Chenge ambapo hatua inayofuata ni kuridhiwa na kusainiwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli ili uwe Sheria kamili ya nchi.

Katika Mkutano huo wabunge walijadili Muswada kifungu kwa kifungu na kuunga mkono upitishwaji wake baada ya Waziri mwenye dhamana na habari kutoa hoja ili Muswada huo uweze kujadiliwa.

Mara baada ya kupitishwa Muswada huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amewashukuru wadau wote walioshiriki katika kutoa maoni juu ya Muswada huo kwani ndiyo yamepelekea kukamilisha mchakato mzima wa Muswada huo.

“Kwa niaba ya Serikali napenda kuwashukuru wadau wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kuhakikisha tunatimiza malengo ya takribani miaka 20 iliyopita ya kuifanya taaluma hii ya habari kuheshimika kama zilivyo taaluma zingine” – Waziri Nape.

Nape amesema, kwa sasa Muswada huo umeshapitishwa hivyo kilichobaki ni utungaji wa Kanuni ambapo ameomba wadau wa tasnia ya habari kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa maoni yatakayopelekea kuwa na kanuni zenye tija kwa wanahabari na taifa kwa ujumla.

Waziri huyo pia amewaasa wadau wa habari kuunganisha nguvu kwa pamoja hasa katika kipindi hiki ambacho Muswada huo umepitishwa pia amewataka wadau hao wasiruhusu mgawanyiko utokee kati yao bali washirikiane na Serikali katika kutekeleza wajibu wao wa kihabari kwa jamii.

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju amesema kuwa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 ni mwanzo mpya wa tasnia ya habari nchini.

Masaju amewaasa wadau wa habari wakiwemo waandishi wa habari kutambua kuwa haki mara zote huendana na wajibu, hivyo hakuna haki isiyo na wajibu.

Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 uliopitishwa leo umejadiliwa na Bunge hilo kwa siku mbili, kwa mara ya pili ulisomwa mbele ya Kamati ya Bunge zima na hatimaye kusomwa kwa mara ya tatu ili kukidhi hatua za utungwaji wa Sheria nchini.

Video Mpya: Ommy Dimpoz & Ali Kiba - Kajiandae
Pacquiao kuzichapa na Vargas saa chache zijazo, ni pambano lililobeba historia