Ndoto za kiungo kinda wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Dele Alli za kucheza hadi mwishoni mwa msimu huu huenda zikaingia kizani, kufuatia ushahidi uliothibitishwa na chama cha soka nchini England FA.

FA wamepata ushahidi wa utovu wa nidhamu ulioonyeshwa na Dele, baada ya kujiridhisha kiungo huyo kumsukuma na kumpiga kiungo wa West Bromwich Albion, Claudio Yacob wakati wa mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England uliochezwa mwanzoni mwa juma hili na kushuhudia matokeo ya sare ya bao moja kwa moja yakipatikana.

Kitendo hicho hakikuonwa na mwamuzi Mike Jones aliyechezesha mchezo huo, hatua ambayo ilitoa msukumo kwa FA kurejea picha za televisheni na kubaini kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20 alifanya kosa hilo kwa makusudi.

Kosa hilo linaweza kumsababishia adhabu Alli ya kufungiwa michezo mitatu na chama cha soka nchini England FA.

Kama itakuwa hivyo, huenda mambo yakawa magumu kwa meneja wa Spurs, Maurico Pochettino katika michezo mitatu ya mwishoni mwa msimu huu, kutokana na mipango yake kumuhitaji sana Dele.

Picha ya ushahidi inayoonyesha Dele Alli Akimsukuma na kumpiga kwa makusudi kiungo wa West Bromwich Albion, Claudio Yacob

Dele ambaye alitangazwa kuwa mchezaji bora mwenye umri mdogo msimu huu kupitia tuzo za chama cha wachezaji wa kulipwa nchini England (PFA) mwanzoni mwa juma hili, ameonyesha uwezo mkubwa na kufanikisha azma ya Spurs kuwa sehemu ya kuwania ubingwa.

FA wanatarajia kutangaza adhabu kwa Dele, wakati wowote kuanzia sasa.

Spurs imesaliwa na michezo mitatu kabla ya msimu huu haujafikia kikomo, ambapo mwanzoni mwa juma lijalo watapambana na Chelsea katika uwanja Stamford Bridge, kisha watarejea nyumbani White Hart Lane kupambana na Southampton kabla ya kumaliza msimu kwa kupambana na Newcastle United ugenini.

Muswada kuhusu zuio la Ndoa kwa hawa... kutua bungeni
Miss Tanzania, Aliyekuwa Kamishna wa TRA, waanza kupeta mahakamani