Aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Edna Lema amesema kuwa anaamini atakuwa kocha wa kwanza mwanamke kuinoa timu ya Ligi Kuu Bara kwa kuwa anaamini uwezo anao wa kufanya hivyo.

Edna maarufu kwa jina la Mourinho, ameyasema hayo baada ya kutambulishwa kuinoa timu ya wanaume ya Mkwabi FC inayoshiriki michuano ya Kombe la Ramadhan inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema ni muda mrefu amekuwa akitamani kuinoa timu ya wanaume bila ya kujali ni mashindano gani baada ya kukaa kwenye soka la wanawake kwa muda mrefu, lakini sasa anaamini pia iko siku atatimiza ndoto yake ya kutua Ligi Kuu.

“Mimi nafikiri katika kazi ya ukocha ni kuishi na kujifunza, yawezekana kila kitu mwanzo ni kigumu lakini unawezakuona ugumu sababu uko nje, ukiwa ndani utaona sababu hata kwa wanawake kuna ugumu pia lakini kwangu mimi nimeona hata kufundisha wa kiume ni rahisi.”

“Natamani kuona siku moja na ninaamini nitakuwa kocha wa kwanza mwanamke kufundisha timu ya wanaume, kwangu natamani hata kesho nipate timu ya Ligi Kuu Tanzania aidha kocha msaidizi au kocha mkuu, naamini uwezo ninao, sitaki kujiweka kwenye nafasi ya siwezi,” amesema Edna.

Amesema kuwa anaamini kila kitu ni kujifunza na hata timu anayoinoa sasa imempa mwanga kwa namna wanaume wanavyoitikia na kusikiliza mafunzo yake na hata namna anavyowasiliana nao.

Zaidi ya Milioni 1 waathiriwa na magonjwa ikiwemo Kipindupindu
Doumbia afunguka kinachomkwamisha Young Africans