Meneja wa Klabu Bingwa nchini Hispania FC Barcelona, Xavi Hernandez amesema uwezekano wa Lionel Messi kurejea katika klabu hiyo ya Katalunya msimu ujao inategemea sana nia ya mshambuliaji huyo wa Argentina.

Messi anamaliza mkataba na klabu ya Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu huu, huku vyanzo vya habari vikiiambia ESPN kwamba ataachana na klabu hiyo ya Ufaransa.

Messi anavutiwa na klabu za Saudi Arabia na Marekani, lakini Barca wana matumaini ya kumrejesha licha ya matatizo ya muda mrefu ya kifedha ambayo yalisababisha kuondoka kwake mwaka 2021.

“Ni suala la hali itakuwaje,” amesema Xavi katika mkutano na waandishi wa habari alipoulizwa kuhusu nafasi ya Barca kumsajili Messi.

“Inategemea mambo mengi. Sina mengi zaidi ninaweza kusema, Messi ni mwanasoka wa kuvutia. Ni rafiki. Kutoka hapo, inategemea mambo mengi, lakini juu ya yote nia yake na kile anachotaka.”

Messi, ambaye anatimiza umri wa miaka 36 Juni, anaweza kulipwa kiasi kikubwa zaidi nchini Saudi Arabia, lakini haiba ya Barca kumrejesha imeongezeka katika wiki za hivi karibuni, huku makamu wa Rais Rafa Yuste pia akieleza nia yake ya kutaka kumsajili.

“Nataka arudi, huo ndio ukweli,” amesema Yuste akiiambia DAZN Jumamosi baada ya Barca kukabidhiwa kombe la Ligi Kuu ya Hispania, LaLiga, kwenye uwanja wa Spotify Camp Nou.

“Baada ya kila kitu alichoipa klabu hii, akipitia akademi, akianzia kucheza hapa ni hadithi nzuri na hadithi nzuri lazima ziwe na mwisho wa furaha.

“Ikiwa kila kitu kitaenda sawa na hata kama atalazimika kufanya uamuzi wa mwisho natumaini atarejea. Sote tutafurahi sana,” amesema Xavi

Barca wamewasilisha mpango wa kutekelezwa kwa La Liga wakieleza kasoro watakazofanya katika kipindi cha miaka miwili ijayo ili kusajili mikataba mipya inayotolewa kwa wachezaji wa sasa wa kikosi cha kwanza, akiwamo Ronald Araujo na Gavi, pamoja na kufanya usajili msimu huu wa majira ya joto.

Barca wamekosa beki wa kulia katika kipindi cha pili cha msimu, lakini Xavi amesema kipaumbele ni kutafuta mbadala wa Sergio Busquets, ambaye ameamua kutoongeza mkataba wake na klabu hiyo.

“Beki wa kulia sio kipaumbele nambari moja,” amesema bosi huyo wa Barca.

“Busquets anakwenda kwa hivyo ni dhahiri tunahitaji kiungo wa ulinzi wa kiwango cha juu kwa msimu ujao.

“Nahodha wetu anaondoka, hivyo tunahitaji mchezaji mzuri sana ili aingie, tunapaswa kuchukua nafasi yake kwa njia bora zaidi, kutoka hapo, kuna vipaumbele vingine na tunapoimarisha zaidi, tunataka kuwa na ushindani zaidi.”

ESPN iliripoti Machi kwamba, Inigo Martinez, Ilkay Gundogan na Ruben Neves ni miongoni mwa wachezaji wengine wanaotarajiwa kusajiliwa msimu huu wa majira ya joto pale Barca.

TANAPA yatoa ufafanuzi tukio la vurugu Mto wa Mbu
Mamilioni yatumika kukarabati miundombinu vikosi, makambi