Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, ametoa kauli nzito kuhusu kinachoendelea nchini katika vyama vya siasa hususan upepo wa viongozi kuhama vyama na siri iliyo nyuma ya matukio hayo.

Mzee Butiku alitoa kauli hizo jana katika mdahalo ulioandaliwa na taasisi hiyo na kufanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Kutokana na uzito wa kauli za Mzee Butiku pamoja na hali ilivyo nchini kisiasa, Dar24 tumeamua kukuandikia kila neno alilosema bila kuongeza wala kutafsiri.

Hivi ndivyo alivyosema Joseph Butiku:

“Mwalimu alipenda CCM imeguke. Na alisema hivyo mara nyingi, hata aliposema CCM sio mama yangu. Mwaka 1992, wakati tunaanzisha [vyama vingi], Mangula nadhani utakuwa unakumbuka. Akasema, ‘isiwe mwiko wala isiwe taboo, kama watu wako humu ndani ya Chama Cha Mapinduzi. Isije ikawa dhambi kwa wale wanaotaka kutoka humu

“Mwalimu alisema, ‘maadam tunakwenda kwenye vyama vingi. Kama unaona unatofautiana na CCM, unaweza kutoka’. Kosa walilofanya hao wanaotoka sasa na wnaotoka sasa, ni kubaki ndani ya chama kile kwa miaka yote hii wakati hawakubaliani nacho. Mmenielewa? Hayo sio maadili, unakaa katika nyumba ya watu na haukubaliani nayo na hutoki, na unavuruga.

“Hoja sio utajiri, hoja ni unavyotumia utajiri wako. Last time niliwaambia Chama Cha Mapinduzi kilikuwa na kundi la watu wachache wanaitwa ‘mtandao’. Na nitarudia hapa, mjue nchi yenu, msikae mnalala tu usingizi.

“Mtandao una watu wasiopungua kumi, na hao waliohama chama wamo. Hawakubaliani nacho, wanasema ndani kuna mizengwe. Na maana ya mizengwe ni kile wanachosema hawataki utaratibu, hawataki waulizwe maswali, wanataka horela. Pili, wanasema ‘tunachelewa kutajirika’. Sasa kama walikuwa wanajua hivyo kwa nini wasingetoka 1992? Nyerere aliwaruhusu mapema. Lakini wanategea, hawataki utaratibu na wanaendelea.. na walianza kabla ya mwaka 1990, wanavuruga chama hiki na wanatumia vijana ninyi. Vijana, vijana, vijana.

“Hata rais alipochaguliwa, aliposimama Morogoro alikuwa amewaahidi vijana. Walimsimamisha pale wakamwambia tumechoshwa na umasikini na tumechoshwa na kunyanyaswa. Ndio ikaja hii ‘Maisha Bora..sijui na nini’, sasa vijana na leo ni bora? Ahadi zisivyo!

“Kwa hiyo watu hawa wameendelea kukaa ndani ya Chama Cha Mapinduzi na wameharibu chama kile. Chama kile ni kama kimejijengewa mazingira ya kunuka!

Chama hiki kimeendesha hii nchi kwa miaka zaidi ya 54. Sitaki kukitetea kwa sababu juzi nilisema mkituletea uchafu tutawaambia watanzania watupigie kura.

Chama kimevurugwa kwa ajili ya hao. Nataka mjue mambo haya, watu waliojipachika katika maeneo ambayo hawakubaliani, sasa wakati umefika wakaondoka.

“Na mimi nawaambia, Profesa Baregu mimi nashukuru wapokee. Ni watu safi hawataki mizengwe, wanataka kutajirika. Na huo ni msimamo sawa tu hauna makosa. Lakini wasijifiche ndani ya vyama vingine na wakaenda kuvuruga mule. Kwa hiyo ninyi [vyama vya siasa] tazameni maslahi yenu.

“Wala simsemi Edward wala simsemi nani.. nikisema mambo ya Edward nayafahamu mengi tu, kama anavyofahamu ya kwangu. Sina haja ya hiyo, nasema la msingi. Kama hukubaliani na msimamo, unatoka mara moja. Sio kuchafua nyumba za watu halafu unatoka.

“Mtandao ulikuwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi, na Mangula mmeuvumilia mno, siku nyingine msifanye hivyo. Sasa unaona unasumbua. Sasa hivi nimepata information hapo, sijui kama ni ya kweli.. mmoja wa mawaziri wa zamani wanasema kuwa hiki chama kina uchwara..sijui kina nini..

“Sasa utajiri na uongozi, jambo langu la mwisho. Nani amesema utajiri ni mbaya? Baba wa taifa alisema siku zote utajiri ni mzuri, usitumiwe kama Marekani wanavyotumia kutukandamiza sisi. Usitumiwe utajiri ukakandamiza wanyonge. Utajiri unatupia pesa zetu chini..! watoto wanaangukiana. Unatupa fedha chini kama unatupia kuku! Watoto wenu wanaangukiana kwenye mapikipiki.. wanaanguka chini! Hayo mkifanya UKAWA tutasema hawafai.

“Tumeshawaambia CCM mlifanya hayo mlifanya makosa. Na ni vizuri mkawaambia watanzania mlikosea. Ni chama kikubwa, hakuna kasoro ya kusema mtusamehe. Watanzania wamebabaika muda mrefu na wanababaika sasa. Vijana hawa wa mtandao, mwaka 1995 walitafuta uongozi huohuo, wakakosa. Walikuwa wanatabia hiyo mbaya-mbaya. Walikwenda mbele ya Mwinyi, mbele ya Mwalimu Nyerere, hawataki utaratibu wakaenda kumgomea Mwinyi pale. Nini mnataka mashtaka, Profesa [Baregu] unataka mzee Mwinyi atoke kumshitaki Lowassa…na Kikwete? Mataifa yenu ni machanga, yapo mambo mengine mnaacha. Aliyemshitaki Edward alikuwa Mwinyi. Mnajua hilo? Juzi Edward ametengeneza… mmeshaona mahali rais anafika halafu mmegomesha watu wanaimba mtu mwingine!? Ninyi ni watu wa ajabu sana. Hivi huyu kijana muungwana sana huyu rais Kikwete. Hivi angekasirika akasema ‘tunafunga mkutano’. Na akaenda akamkamata yule akaenda akamfunga, ingekuwaje?

“Wewe unaweza kwenda kwenye kikao ukakuta umepinduliwa? Siasa gani hizi! Muendelee na demokrasia, na itawala. Mimi ni mzee nawaambieni sitaki kuwalaani, muendeleeni na demokrasia ya kihuni. Na itawamaliza. Asanteni sana. Sasa naomba tufunge.”

Murray Kidume Rogers Cup
Mabasi Yaendayo Kasi Kuanza Kazi Leo Dar, Abiria Kupanda Bure