Mbunge wa Mwibara, Kangi Logela (CCM) amekosoa vikali kitendo cha Serikali kupitia Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/17 iliyowasilishwa bungeni, kukata kodi kwenye kiinua mgongo cha Wabunge.

Akichangia katika mjadala wa Bajeti Bungeni, Kangi Lugola ameeoesha kushangazwa na uamuzi huo ambao amedai utawarudisha nyuma wabunge kifedha kwani wamekuwa wakitumia pesa nyingi katika shughuli za wananchi Bungeni huku wakipokea maombi lukuki ya fedha kutoka kwa wananchi wao.

“Sisi wabunge, kule mtaani kule ndio ATM. Hata sasa hivi huku kila simu ya Mbunge… ‘sijui kuna msiba wapi, sijui kuna kisima kimeharibika, sijui kuna darasa upepo umeezua’, ndipo hapohapo tunapotoa pesa,” alisema Kangi Lugola.

Alisema kuwa alitegemea Serikali ingewasilisha muswada wa sheria wa kufuta kodi kwenye kiinua mgongo kwa watumishi wote kwani walishakatwa kwenye mishahara yao kwa kipindi cha miaka 40 walioyokuwa wakitumikia Serikali, lakini ameshangaa hata wabunge wanaowatetea sasa wamewekewa kodi.

Lugola alisema kuwa hali hiyo itawarudisha wabunge kwenye hali ngumu ya maisha kutokana na namna wanavyotumia fedha zao kwa wananchi huku akikumbusha kuwa aliyewahi kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda alieleza wazi kuwa wapo wabunge waliopita waliogeuka kuwa wanaomba fedha za kujikimu.

“Ninyi wenyewe ni mashahidi, akiwepo Mheshimiwa Makinda hapa. Alisema amechoka kusumbuliwa, wabunge ambao walishastaafu wamekuwa wakija ofisini wanamuomba hela, wamekuwa ombaomba. Waheshimiwa wabunge, leo maslahi yetu tumedunduliza na tumekatwa kodi ya mapato kila mwezi, halafu tena mafao yetu ambayo yamelimbikizwa na yenyewe yakakatwe kodi!? Mnataka turudi mitaani ili muanze kutucheka?” Alihoji.

 

Video: Kama unamiliki simu ya Tecno haya hapa mambo ya kufahamu kutoka Tecno
Mwanamuziki wa Marekani auawa kwa risasi kwenye tamasha lake