Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea amesafirishwa kwa ndege leo Jumatano asubuhi kwenda Dodoma anakohitajika mbele ya Kamati ya  Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Mbunge huyo jana Jumanne alisema alikuwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay Wilayani Kinondoni akisubiri utaratibu wa safari hiyo ya kwenda kuhojiwa kama Spika wa Bunge Job Ndugai alivyoagiza.

Katibu wa wabunge wa Chadema, David Silinde akizungumzia safari ya mbunge huyo amesema, Kubenea amesafirishwa kwa ndege asubuhi kwenda Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa na kamati ya Bunge.

Aidha, kwa upande Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kuwa hana taarifa mpya lakini alitakiwa kuondoka leo asubuhi kwa ndege.

Hata hivyo, Kubenea amepelekwa mbele ya kamati ya Bunge akituhumiwa kwa taarifa alizozitoa kupitia mitandao ya kijamii kuwa Spika alisema uongo kuhusu idadi ya risasi alizopigwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu katika tukio lililotokea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma Septemba 7

LIVE: Rais Magufuli akihutubia wananchi Manyara
Mpina: Serikali haitawavumilia wawekezaji