Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa amelazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kufanyiwa upasuaji wa tumbo.

Taarifa kutoka kwa familia hiyo zinasema kuwa kiongozi huyo amelazwa katika hospitali hiyo kwa karibu wiki nzima baada ya kupata hitilafu iliyotokana na kufanyiwa upasuaji.

Mbunge wa jimbo la Monduli, Fredrick Lowassa ambaye ni mtoto wa Lowassa amesema kuugua kwa baba yake sio swala la siri na watanzania waendelee kumuombea.

“Baba alilazwa kama siku tano zilizopita. Wala haina siri, alifanyiwa upasuaji wa tumbo, lakini bahati mbaya ikaleta complication (hitilafu). Alifanyiwa hapo hapo Muhimbili,” amesema Fredrick.

Amesema wanaomba watanzania, kuendelea kumuombea ili afya yake iendelee kuimarika.

“Tunashukuru sana kwa maombi ya Watanzania na tuna imani ataruhusiwa kurejea nyumbani,” amesema.

Hivi karibuni Waziri huyo mkuu mstaafu amekua kimya na kutosikika katika majukwaa ya siasa na sehemu mbalimbali za kijamii.

Rapa Big Sean athibitisha kuwa na asili ya Nigeria
Ajali ya lori yauwa wawili Dar es Salaam