Meneja wa klabu bingwa nchini Hispania FC Barcelona, Luis Enrique amesema hana mikwaruzano na walinda mlango wa klabu hiyo.

Claudio Bravo pamoja na Marc-Andre ter Stegen kwa pamoja waliwasilisha malalamiko yao kwenye uongozi wa Barca, wakikiri kutokua na furaha na sera inayotumiwa na meneja huyo kutoka nchini Hispania za kuwabadili kikosini mara kwa mara.

“Tuna walinda mlango watatu ambao wana uwezo unaoshabihiana, hivyo sina budi kuwatumia kwa uangalifu mkubwa ili kila mmoja aweze kushiriki kikamilifu katika majukumu ya kuitumikiwa FC Barcelona.

“Sina hofu yoyote endapo mmoja wao atahitaji kuondoka, lakini kwangu naamini sera ya kuwatumia kwa kumpa kila mmoja nafasi ndio bora zaidi.” Alisema Luis Enrique alipozungumza na waandishi wa habari nchini Marekani

Katika hatua nyingine, Enrique ameonyesha kufurahishwa na uwezo wa mshambuliaji kinda Munir El Haddadi, ambaye amekua akimtumia kama mchezaji wa akiba tangu alipokabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa benchi la ufundi miaka mitatu iliyopita.

“Ninamuamini Munir, ana uwezo mkubwa wa kucheza soka na kufunga mabao. Bado ni kijana mdogo na anatakiwa kuendelezwa kwa kupewa nafasi kila inapowezekana.” Alisisitiza Enrique

Kikosi cha FC Barcelona usiku wa kuamkia hii leo kilicheza mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya mabingwa wa soka nchini England Leicester City, na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao manne kwa mawili.

Video: Taarifa kuhusu Rais wa Simba Aveva na wenzake watatu kushikiliwa na Polisi
Manispaa Morogoro yapewa siku moja kutenga maeneo ya Wafanyabiashara wadogo