Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amemuandikia barua kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis akimuomba kuingilia kati kwa kutumia ushawishi wake kutatua mgogoro wa Zanzibar kwa amani.
Barua hiyo imebainika kuwa iliandikwa Novemba 25 mwaka jana, ambapo Maalim Seif alimuelezea papa Francis kuhusu hali ya kisiasa nchini Zanzibar na kinachoendelea kuwa kinaweza kupelekea hali mbaya.
“Ni wiki tatu sasa tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu na hali hii imesababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli za kuichumi kutokana na wananchi wengi kuwa na hofu kuhusu mustakabali wa hali hii….watu wanashindwa kujua nini kitatokea maana wana hofu kwamba hali hii inaweza kuharibu umoja wa kitaifa kwa watu kuishi kwa upendo bila kujali dini wala kabila,” Maalim seif aliandika.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar, alimueleza Papa Francis kuwa Zanzibar ni nchi yenye mchanganyiko wa madhehebu mbalimbali ikiwa ni pamoja na waislamu na wakristo wanaoishi kwa amani na utulivu siku zote bila kuwa na hofu.
Alisema kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeungana na wenzao wa Zanzibar kuwatishia wananchi badala ya kukemea na kuchukua hatua dhidi ya kile alichokiita uovu dhidi ya katiba.
Alimueleza Papa Francis kuwa hatua ya wananchi kutopewa haki yao ya kuchagua kupitia kisanduku ikiwa ni baada ya miaka 20, kunaweza kupelekea vijana ambao hawafurahishwi na mwenendo huo, kuamua kutumia njia mbaya kutafuta haki yao.