Rais John Magufuli ambaye leo amelitaja baraza lake la Mawaziri linalotarajiwa kukamilika likiwa na watu 34 pekee, amesema kuwa ameokoa takribani bilioni 2 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya semina elekezi za mawaziri wake.

Akiongea baada ya kulitaja baraza lake, Dk. Magufuli alieleza kuwa kwenye baraza lake hakutakuwa na semina elekezi na kwamba kiasi hicho cha fedha kilichokuwa kimetengwa atakielekeza katika shughuli nyingine.

“Hakuna semina elekezi, hata sisi tulipoapishwa tu tulianza kazi. Waziri Mkuu alijielekeza kwenye bandari, Makamo wa rais nae akajielekeza kwenye usafi wa mazingira,” alisema rais Magufuli.

Aidha, rais Magufuli aliwataka mawaziri wake kutofanya sherehe kwa sababu wameteuliwa kwa kuwa wana kazi kubwa mbele yao.

“Ukifanya sherehe wakati wa kuapishwa, jiandae na kufanya sherehe pia wakati utakapofukuzwa,” alisema.

Hata hivyo, rais bado hajataja mawaziri wa wizara nne ambazo ameahidi kuwatangaza siku za usoni.

 

 

Petr Cech Anena Baada Ya Ushindi Dhidi Ya Olympiakos
Wanalizombe Wamrejesha Mrwanda Ligi Kuu