Mashetani wekundu (Man Utd) wametenga kiasi cha Pauni milioni 70 kwa ajili ya kumsajili kiungo mchezeshaji kutoka nchini Ureno na klabu ya AS Monaco ya Ufaransa Bernardo Mota Veiga de Carvalho e Silva.

Man Utd wameanza kujihami kwa kutenga kiasi hicho cha pesa, kutokana na kutambua huenda wakakutana na upinzani wa usajili wa mchezaji huyo ambaye yupo kwenye mipango ya klabu ya Real Madrid.

Jose Mourinho anaongoza vita ya usajili wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22, na anashinikiza mpango huo ukamilishwe katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, kwa kuhofia purukushani za mwishoni mwa msimu ambapo Real Madrid watakua wamemaliza kifungo cha usajili.

Dhumuni la Man Utd la kutaka kumsajili Bernardo ni kutengeneza mazingira ya kumshawishi mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Atletico Madrid Antoine Griezmann, anaetazamiwa kutua Old Trafford mwishoni mwa msimu huu kwa ada ya uhamisho wa Pauni milioni 85.

Bernardo anaaminika kuwa na uwezo wa kumchezesha mshambuliaji huyo, endapo watakuwa pamoja katika kikosi cha Man Utd msimu ujao.

Bernardo ni mchezaji anaesimamiwa na wakala Jorge Mendes ambaye ni msimamizi pia wa Jose Mourinho, hivyo ukaribu huo unatarajiwa kutengeneza urahisi wa uhamisho wake.

Bernardo alijiunga na AS Monaco akitokea SL Benfica kwa ada ya uhamisho wa Pauni milioni 14 mwaka 2015, baada ya kusajiliwa kwa mkopo mwaka 2014.

FIFA Yamteua Malinzi Mjumbe Kamati Ya Maendeleo
Ombi La Zanzibar Kujadiliwa CAF