Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya wamesema kuwa watachukua hatua kufuatia uamuzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kuwasimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge hadi Bunge la mwaka ujao.

Wabunge hao machachari wa Chadema, wamesema kuwa wanaendelea kushauriana na chama chao kuhusu hatua za kuchukua, lakini nia yao ni kwenda mahakamani kupinga uamuzi huo waliodai ulitolewa kwa upendeleo.

“Tunaangalia taratibu mbalimbali ikiwa ni pamoja na taratibu za kisheria. Pale ambapo tutafanya uamuzi rasmi wa kufungua shauri mtapewa taarifa na mtajua tumefungua shauri mahakama gani na kwa sheria ipi,” alisema Mdee.

Kwa upande wa Bulaya, alisema kuwa Spika Ndugai hakumtendea haki mbunge wa Kibamba, John Mnyika na kwamba alichofanya ni kuwakandamiza wapinzani huku akimuacha yule aliyemuita mbunge huyo kuwa ni ‘Mwizi’.

“Wasitumie fursa hii wakadhani wanaweza wakawaziba midomo wapinzani. Na hii imekuwa desturi kwamba wanaoonewa siku zote ni wabunge wa upinzani. Ametukanwa Mnyika ameitwa ‘mwizi’, na aliyemuita mwizi ni mbunge wa CCM. Lakini spika hasikii sauti nyingine, lakini ile ya Halima Mdee aliisikia,” Bulaya aliiambia Ayo TV.

Spika Ndugai aliamuru Mnyika atolewe nje ya Bunge kwa kosa la kutotii mamlaka halali ya kiti hicho. Wabunge Mdee na Bulaya wao walikutwa na adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia ya kujaribu kuwazuia askari kumtoa nje Mnyika.

Magazeti ya Tanzania leo Juni 6, 2017
Walinzi wa Netanyahu wavutana na walinzi wa Rais wa Togo mkutanoni