Baada ya kupoteza mchezo wa fainali ya Mapinduzi Cup kocha mkuu wa Mtibwa Sugar Mecky Maxime amesema amekubali matokeo ya mchezo huo kwa timu yake kulala kwa magoli 3-1 dhidi ya URA FC ya Uganda na kupoteza fainali ya pili mfululizo ndani ya miaka miwili.

Muda mfupi baada ya kumalizika kwa pambano la fainali, uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo kisiwani Unguja, Maxime alisema, amekubali kushindwa licha ya timu yake kucheza vizuri kwa kiwango cha juu.

“Mchezo wa mpira ndivyo ulivyo, unaweza ukacheza vizuri lakini usipate matokeo unayotarajia. Timu yangu imecheza vizuri lakini tumeshindwa kuibuka washindi wa mchezo wa fainali, mpira unamambo mengi, amesema nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa na timu ya taifa ya Tanzania.”

Maxime aliongeza kuwa, mashindano ya mwaka huu yamekuwa ni mazuri licha ya kuwepo kwa kasoro chache ambazo kama zikifanyiwa kazi na kukirekebishwa itasaidia kuboresha mashindano hayo.

“Mashindano ya mwaka huu yamekuwa mazuri japo kulikuwa na mapungufu ya kawaida ambayo binadamu yeyote anaweza akafanya hata mimi pia pengine ningekosea lakini kama waandaji watayafanyia kazi mapungufu hayo basi huenda mashindano haya yakazidi kuwa bora siku zijazo.”

Fainali kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya URA ilikuwa ni ya tano kwa Mtibwa tangu michuano ya kombe la Mapinduzi ilipoanza mwaka 2007.

Katika fainali zote ambazo Mtibwa imecheza, imefanikiwa kutwaa taji la Mapinduzi mara moja ambapo ilikuwa ni mwaka 2010 ilipoifunga timu ya Ocean View kwenye mchezo wa fainali uliopigwa kwenye uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba.

Gor Mahia Wakamilisha Usajili Wa Nahodha Wa Amavubi
Dylan Kerr: Siondoki Dar es salaam Mpaka Nilipwe Changu