Kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru amekitahadharisha chama hicho kujiepusha na migogoro ya makundi yanayopambana bali wajikite katika kukijenga chama hicho kwa kufuata misingi ya haki.

Kingunge alishangaa nguvu kubwa inayotumiwa na chama hicho kupambana kupitia makundi yaliyoko ndani ya chama kuliko nguvu zinazotumika kupambana na wapinzani.

“Tusipoteze nguvu zetu kubwa kabisa kupambana wenyewe. CCM haiwezi kusimama tunapopambana wenyewe kwa wenyewe, ni barabara ya kutokomea baharini,” alisema Mzee Kingunge.

Kingunge aliipinga vikali kauli ya Katibu Mwenezi na Itikadi wa Chamama hicho, Nnape Nnauye ya kuwataka wagombea ambao majina yao yatakatwa katika mchujo wa kumpata mgombea atakayekiwakilisha chama hicho kuwania kiti cha urais, wasikate rufaaa. Kingunge ameichukulia kauli hiyo kama hali ya kuwanyima wagombea haki ya msingi.

Akijibu hoja zilizotolewa na Mzee Kingunge, Nape Nnauye alitofautiana na mtazamo huo na kueleza kuwa kinachokipasua chama sio migawanyiko katika kutafuta uongozi bali ni tofauti za imani ya chama.

“Kinachopasua chama si migawanyiko katika kutafuta viongozi. Kinachopasua chama ni tofauti za msingi za imani ya chama husika. CCM hii imekuwa na uzoefu wa kupitia michakato ambayo imekuwa na misuguano mikubwa toka mwaka 1995, mwaka 2005 kulikuwa na misuguano ya namna hii katika kumpata mgombea,” Nape aliiambia BBC.

“Mimi nadhani, kwanza kama nilivyosema ni mtazamo wao na ninauheshimu sana. Na kwa sababu ya mapenzi yao makubwa kwa Chama Cha Mapinduzi wanajaribu kutoa tahadhari. Chama hakitapasuka, sioni namna ambayo chama kinapasuka. Haki ikitendeka kwa namna yoyote ile, hakuna namna ambayo chama kitayumba,” aliongeza.

Hayo yanaendelea wakati ambapo siku zinazidi tatu kabla chama hicho kulichagua jina moja la mgombea atakepita kwenye mchunjo wa vikao na ngazi za maamuzi za chama hicho. Kazi inayofanyika mjini Dodoma. Julai 12 mwaka huu, inatarajiwa kuwa siku itakayotegua kitandiwili cha nani anakabidhiwa kijiti kuiongoza CCM katika za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tundu Lissu aizungumzia Barua ya Shibuda Kwa Chadema
Rais Wa FC Barcelona Auchekesha Umma Na Hadhithi Ya Sungura