Katibu Mwenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye ameyabariki majina matano maarufu kama ‘tano bora’ yaliyokuwa yakitajwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa yaliyopitishwa na Kikao Kikuu (CC).

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Nape amesema ni kweli waliochaguliwa kuingia hatua ya tano bora ni Bernard Membe, January Makamba, John Pombe Magufuli, Asha Rose Migiro na Amina Salum Ali.
Nape amewashauri wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya Chama hicho waliojitokeza kupinga matokeo na utaratibu uliotumika kuwapata wagombea hao kuwa wanapaswa kufuata njia sahihi kwa mujibu wa katiba ya chama.

Aidha, Katibu Mwenezi na Itikadi amekanusha taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari kuwa aliwataka wagombea ambao majina yao yatakatwa kutokata rufaa.

Amesema vyombo vya habari vilimnukuu vibaya na kwamba kukata rufaa ni haki ya kila mgombea na sio mara ya kwanza kwa wagombea wa chama hicho kufanya hivyo katika hatua hizo za kuwapata wagombea.

Hata hivyo, suala la muda wa kukata rufaa lilionekana kuwa changamoto kwa wale watakaoamua kufanya hivyo kwa kuwa ndani ya saa 18 uamuzi wa kumpata mgombea mmoja unaweza kuwa umekamilika.
Naye Mh. John Pombe Magufuli, ambaye ni mmoja kati ya waliotajwa kuingia tano bora alitoa ‘neno’ lenye maelezo mafupi alipopita mbele ya waandishi wa habari.

“Asanteni sana, nashukuru… naombeni kura zenu,” alisikika Magufuli.

Kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) unatarajiwa kuanza majira ya saa tano asubuhi kufanya mchujo utakaopata majina matatu yatakayopelekwenye mkutano mkuu wa chama.

Mkutano huo mkuu wa CCM unatarajiwa kuanza majira ya saa nane mchana na kulichagua jina moja litakaloipeperusha bendera ya chama hicho, Octoba 25 mwaka huu. Tarehe itakayotoa majibu ya nani anakuwa rais mpya wa Tanzania.

West Ham Wamnyemelea Zaidi ‘Mnigeria’ Wa Juventus
Newcastle Utd Kuongeza Majembe