Picha halisi ya Oktoba 25 ndani ya kituo cha kupigia na kuhesabia kura inazidi kubadilika tofauti na wengi walivyotajiwa, hii ni baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupiga marufuku mawakala wa vyama vingine vya siasa vinavyounda Ukawa kusimamia kura za mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Uamuzi huo wa NEC umewekwa wazi jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima Kombwey, alipokuwa anaongea na waandishi wa habari.

Kailima alifafanua kuwa NEC haitambui Ukawa bali wanatambua mgombea urais wa Chadema kisheria hivyo mawakala wa Chadema pekee ndio watakaoruhusiwa kusimamia kura za mgombea wao na sio vinginevyo.

“Ataingia muwakilishi wa Chadema. Hatuwezi kusema muwakilishi wa CUF aingie kwa niaba ya Chadema…hapana. Ni chama husika kilichosimamisha mgombea ndio kinaruhusiwa kumpeleka wakala mle ndani,” alisema Kailima.

“Kwa hiyo wasije kuunda huko pembeni kwama CUF aingie kwa niaba ya Chadema, hakuna biashara hiyo. Kama CUF hana mgombea yoyote wa kiti cha udiwani au Ubunge haruhusiwi kuingia mle ndani, unaingia tu kama una mgombea,” aliongeza.

Ukawa inaundwa na vyama vinne vya upinzani ambavyo ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi pamoja na NLD.

Blatter Awagomea Wadhamini Wakuu Wa Fifa, ‘Sijiuzulu’
Angalia Trailer ya mwisho ya Filamu Mpya ya James Bond ‘Spectre’