Mbio za kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu zimekuwa za kihistoria na zenye ushindani mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Tukio la kujiunga kwa vyama vinne vikubwa vya siasa nchini limeweka historia nzuri ya umoja wa vyama vya siasa wenye lengo la kuking’oa madarakani chama tawala (CCM).

Tukio hilo liliongezwa nguvu zaidi baada ya kumkaribisha kada mkongwe wa CCM na waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa aliyekiacha chama chake hicho cha zamani akipinga uamuzi wa chama hicho kuliondoa jina lake katika mchakato wa kura za maoni uliompa nafasi Dk. John Magufuli kupeperesha bendera ya chama hicho kuwania urais.

Jana, vyama hivyo vilikuwa na matukio mawili tofauti yaliyopelekea kusikika sauti za viongozi wa vyama hivyo wakitambiana kwa maneno ya kejeli huku kila kimoja kikitamba kuwa kitashinda kwa kishindo.

Upande wa CCM ambao jana ulimsindikiza mgombea wake wa urais kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo katika ofisi ya tume ya uchaguzi, walitamba kuwa wataibuka washindi kwa kishindo wakiwafunga magoli wapinzani wao kama wamesimama.

Mwenyekiti wa CCM, Dk. Jakaya Kikwete aliwahakikishia wanachama wa chama hicho kuwa watashinda kwa kishindo katika uchaguzi huo kwa kuwa nia na uwezo wa kushinda wanao.

“Wanaodhani CCM ni chama cha mchezo watakiona…Tumejiandaa vya kutosha kushinda, na kushinda tutashinda,” alisema Dk. Kikwete.

“Kinachotakiwa wana CCM ni kujipanga, hakuna kudharau adui hata awe mdogo. Maadam yuko upande wa pili, shughulika naye,” ni kauli nyingine ya Dk. Kikwete.

Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana alipita kwenye mstari uleule wa maneno ya kujigamba aliyoyatoa Mwenyekiti wa chama hicho.

“Sasa ni washukuru sana kwa namna mlivyomsindikiza mgombea na mgombea mwenza kuanza safari ya ushindi, kwenda kwenye tume kuchukua fomu, na leo amekabidhiwa fomu. Safari imeanza, mbele kwa mbele na wataisoma namba,” alitamba Abdulrahman Kinana.

“Bahati nzuri tunashindana na makapi ya CCM,” Kinana alisema kwa kejeli na kuongeza kuwa hawawezi kushindwa na makapi.

Naye mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli alibeza nguvu ya wapinzani wake akidai kuwa haoni mtu wa kumshinda kwenye uchaguzi huo na kwamba lazima watashinda kwa kishindo.
Magufuli mbele

Kwa upande wa Ukawa, jana viongozi wa umoja huo walihudhuria Mkutano Mkuu wa Chadema uliobariki jina la mgombea walitoa kauli za tambo na majigambo kuwa mwaka huu lazima waishike dola na kuking’oa Chama Cha Mapinduzi madarakani.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa mpango wa kuingia ikulu ulifanyiwa utafiti na kupigiwa mahesabu kisayansi kabla ya kukubali kumkaribisha Edward Lowassa kuwa mgombea wao hivyo lazima watashinda.

“Kuna mbunge wetu mmoja anapenda kusema ‘numbers don’t lie’,” alisema Mbowe na kusisitiza kuwa lazima mwaka huu CCM wataondoka madarakani.

Hotuba ya shukurani ya Edward Lowassa pia ilijaa tambo na majigambo kuwa lazima watashinda na kushika dola.

“I came to join you for a reason, kuwaondoa CCM madarakani ..Tutachukua dola Oktoba 25 asubuhi…niliwahi kuwaambia waandishi wa habari kuwa mimi sina msamiati wa kushindwa, lazima tutashinda,” alisikika Edward Lowassa akitamba katika hotuba yake.

Lowassa aliwaahidi makada wa Chadema kuwa atahakikisha anafika kila jimbo la uchaguzi ili kuongeza nguvu ikiwa ni mkakati wa kushinda kwa kishindo.

“Nataka kuwaahidi kuwa nitapita kila jimbo la nchi hii, kwa hiyo unapoondoka hapa kajiandae katika jimbo lako, ‘I will come’.

Naye mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad alitamba kuwa lazima ataingia ikulu mwaka huu na kwamba dola itashikwa na umoja huo wa upinzani Bara na  Visiwani bila wasiwasi.

Chadema mbele

Tambo na majigambo ya kisiasa kati ya pande hizi mbili zenye nguvu kubwa zitapata majibu Oktoba 25 mwaka huu pale wananchi waliojiandikisha watakapopiga kura na kufanya maamuzi yatakayokuwa maamuzi ya mwisho.

 

 

Daktari Wa Aspetar Afichua Siri Ya Di Maria Na PSG
Benzema Aendelea Kushawishi Usajili Wake Arsenal