Wakala wa mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Urusi Denis Cheryshev amebadili upepo wa mazungumzo, kwa kuziacha solemba klabu za Arsenal pamoja na Liverpool ambazo zinatajwa kumuhitaji mchezaji huyo kutoka Villareal.

Wakala wa Cheryshev, ameripotiwa kuanza mazungumzo na viongozi wa klabu ya Real Madrid tangu jana, huku akiwa na matumaini ya kumpeleka mchezaji wake katika ndoto za mafanikio za kucheza kwenye klabu iliyomkuza tangu akiwa na umri mdogo.

Meneja wa klabu ya Villareal, Marcelino García alitobia siri hiyo alipozungumza na baadhi ya vyombo vya habari kwa kusema, kuna uwezekano mkubwa kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 akarejea Real Madrid katika kipindi hiki.

Cheryshev, kwa kipindi kirefu amekua akicheza nje ya klabu ya Real Madrid kwa mkopo, kufuatia mazingira ya kikosi cha kwanza cha klabu hiyo, na sasa ameonyesha dhamira ya kweli ya kupambana na wazoefu.

Mwaka 2012, Cheryshev alipandishwa rasmi kuitumikia timu ya Real Madrid ya wakubwa lakini hakuwa na mafanikio na badala yake alipelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya Sevilla na kisha Villareal.

Arsenal na Liverpool zote za nchini England, zilitajwa kuingia kwenye vita ya kumuwania Cheryshev kutokana na kiwango kizuri alichokua akikionyesha akiwa na Villareal, lakini kwa mpango uliopo sasa, hawana budi kuangalia pengine ili kutimiza azma waliokua wamejipangia.

FC Barcelona Kuwatosa Man Utd?
Klopp Aikataa Ofa Ya Olympic Marseille