Kiungo wa klabu ya Arsenal Mesut Ozil ameachwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani ambacho kitaingia kambini mwanzoni mwa juma lijalo, kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za 2018 dhidi ya Ireland Ya Kaskazini na Azerbaijan.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28, ameshindwa kucheza mfululizo kwenye kikosi cha Arsenal tangu aliporejea klabuni hapo mwanzoni mwa mwezi huu akitokea kwenye kikosi cha Ujerumani.

Hata hivyo hali hiyo ilisababishwa na majereha ya goti ambayo yalimsababishia kukosa utimamu wa mwili.

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Low amewaambia waandishi wa habari kuwa, Ozil na kiungo wa klabu bingwa nchini Italia Juventus FC  Sami Khedira, amewaacha kutokana na kukosa sifa ya kucheza mara kwa mara kwenye vikosi vya klabu zao.

Low amesema kuachwa kwa viungo hao hakumaanishi wamepoteza muelekeo ya kukitumikia kikosi chake, bali kupumzika kwao huenda kukawa na faida kwa michezo itakayofuata baada ya mwezi Oktoba.

Wengine walioachwa kwenye kikosi cha Ujerumani ni mlinda mlango Manuel Neuer, beki wa pembeni Jonas Hector na mshambuliaji Mario Gomez ambao wote ni majeruhi.

Katika hatua nyingine kocha huyo ametetea uamuzi wake wa kuwaita Julian Draxler, Thomas Muller na Lars Stindl kwenye kikosi chake huku wakiwa na sifa zinazoshabihiana wanapokua uwanjani, kwa kusema amefanya hivyo kwa makusudi ya kutaka kutumia mfumo mpya katika michezo dhidi ya Ireland Ya Kaskazini na Azerbaijan.

Wakati Ozil akiachwa mchezaji mwenzake kutoka Arsenal Shkodran Mustafi amejumuishwa kwenye kikosi hicho, sambamba na Antonio Rudiger wa Chelsea, Emre Can wa Liverpool na Leroy Sane wa Manchester City.

Timu ya taifa ya Ujerumani ambayo ndio bingwa mtetezi wa fainali za kombe la dunia, tayari imeshafuzu kucheza fainali za 2018, kwa kuweka rekodi ya kushinda michezo minane na kufunga mabao 35 huku wakifungwa mabao mawili pekee.

Halmashauri nchini zaagizwa kurudisha fedha za miradi
Ripoti ya PPRA kutinga bungeni, taasisi 17 kuburuzwa Takukuru