Serikali imedhamiria kuanzisha chombo cha kuendesha na kudhibiti sekta ndogo ya usafiri wa majini, usalama wa meli na mazingira ya bahari ili kulinda maslahi mapana ya taifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati akijibu hoja ya Serikali kuhusu Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwenye kikao kilichofanyika mjini Dodoma.

Prof. Mbarawa amesema kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kupeleka Muswada Bungeni wa kutunga sheria ambayo itaanzisha Shirika  la Wakala wa Meli wa Taifa (NASAC)  ambao utasimamia usalama wa meli na bahari kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa bandari.

“Serikali imeona ianzishe chombo kingine ili kiweze kujikita kusamimia masuala ya usafiri wa majini pekee na masuala nyeti hasa ya uchumi wetu kama vile madini, Chombo kimoja cha kutoa huduma na kudhibiti sio jambo geni. Hapa nchini tunayo taasisi ya Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA) ambayo inatoa huduma ya anga na kudhibiti anga, hivyo Serikali inataka kufanya hivyo pia kwenye sekta ya usafiri wa majini,”amesema Prof. Mbarawa

Aidha, ametoa wito kwa wadau kushirikiana na Serikali kuanzisha chombo hicho. Pia amefafanua kuwa SUMATRA haitapokonywa majukumu yake bali nia ya Serikali ni kuitaka SUMATRA isimamie sekta ya nchi kavu tu kwa maana ya barabara, reli, magari ambayo ni sehemu kubwa na ina changamoto ambayo inahitajika kutatuliwa hivyo ijikite huko.

Hata hivyo, kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla amesema kuwa azma ya Serikali ni nzuri katika muendelezo wa kuhakikisha kuwa taasisi zinazoanzishwa zina mgusa mlaji na kwa manufaa ya Serikali kwa ujumla.

 

Dkt. Mashinji: Waliohamia Chadema wameokoka
Serikali yazionya kampuni za usambazaji pembejeo