Tanzania imeihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kwamba itaendelea kuwekeza rasilimali fedha kwa ajili ya kuendeleza sekta ya elimu, ili kuwa na jamii iliyoelimika kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Ahadi hiyo imetolewa mjini Dubai na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba kwenye kilele cha mkutano unaohusu uwekezaji kwenye sekta ya elimu katika karne ya 21 hasa baada ya janga la UVIKO – 19 kulitikisa nchi nyingi duniani.

Dkt. Nchemba amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuongeza bajeti kwenye sekta ya elimu kila mwaka kadri rasilimali fedha inavyopatikana, na kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kuchangia juhudi hizo za Serikali.

Ameongeza kuwa kipaumbele cha Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa kila mtoto anayetakiwa kwenda shule anapata elimu bila vikwazo kwa kutoa elimu bila malipo huku ikiboresha mazingira ya shule nchini kote.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Tanzania kuna utashi wa kisiasa wa kuendeleza elimu, ambapo bajeti ya elimu imekuwa ikiongezeka kila mwaka na mpaka sasa imefikia zaidi ya asilimia 17 na kwamba huenda siku zijazo ikafikia asilimi 20 ya bajeti yote ya Serikali.

Mkutano huo unaohusu uwekezaji kwenye sekta ya elimu katika karne ya 21 hasa baada ya janga la UVIKO – 19 unajulikana kama WirED, umeshirikisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka duniani kote ambapo hoja mbalimbali za kuboresha elimu, ikiwemo kuwawezesha vijana na kuimarisha masuala ya teknolojia zimejadiliwa kwa kina.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Disemba 15, 2021
Dkt Ndumbaro aruhusu kusafirishwa tani 1683 za gundi kwenda nje