Na Zitto Kabwe.

Jana nimefarijika kukusikia tena sauti yako tangu nikusikie nilipokuja kukusabahi hospitalini. Sauti yako sasa imeboreka na kurudi sauti ile ile uliyokuwa nayo kabla hujashambuliwa kwa risasi nyumbani kwako Dodoma. Watanzania wamefarijika sana kuwa bado uko hai na utaweza kuungana nasi tena kuendeleza mapambano ya kujenga demokrasia yetu.

Siku ile nimekuja kukusabahi uliniuliza nini kinaendelea nyumbani. Nilikwambia tu Watanzania wanakuombea. Ukanitazama kwa lile jicho lako la kiMarx, ukacheka na kusema “Taifa la Waomba Mungu”.Tukacheka. Ni kweli Watanzania wamekuombea sana, na ni jambo la kushukuru kuwa Mola amewasikiliza maombi yao.

 

Ninafuraha kuwa unaendelea vizuri sana tofauti na nilipokuja kukuona. Tutazidi kumwomba Mola afya yako iimarike zaidi. Tuna kazi kubwa sana mbele ya safari, na kwa hakika ni lazima tuifanye kwani tusipoifanya nchi yetu itaanguka kiuchumi na kidemokrasia, na watu wetu kuendelea kuwa maskini zaidi kuliko ilivyo sasa.

Ilikuwa ni lengo la waliokushambulia kutunyamazisha. Tumewaambia kuwa hatutanyamaza kamwe. Kama ulivyoniambia ukiwa kitandani kuwa “tumeshashinda. Tutashinda”. Hakika ushindi ni dhahiri na ndio maana wanatapatapa kuzuia uhuru wa mawazo na fikra.

Ndugu yangu, nisikuchoshe na barua ndefu kwani najua bado hujawa na nguvu za kutosha. Nilikuletea kitabu nikamwambia mkeo awe anakusomea. Naamini anafanya hivyo. Juzi tulisherehekea miaka 50 tangu kuuawa kwa komredi Che Guevara. Najua unavyompenda Che tungekutana ubalozi wa Cuba hapa Dar siku ile.

Shambulio la kutaka kukuua limetuonyesha watu wanaoumizwa na ‘INJUSTICE’ na wasioumizwa nayo. Wengi wasioumizwa na ‘Injustice’ wanadiriki hata kuhoji kwa nini eti tunapaza sauti kuhusu suala lako. Jibu letu kwao ni nukuu hii ya komredi Che Guevara, nukuu ambayo huniongoza katika maisha yangu ya mapambano ya haki.

“If you tremble with indignation at every injustice, then you are a comrade of mine” (Kama unaumizwa na kila uonevu, popote pale duniani, basi wewe ni mwenzangu).

Aahh! Ndugu yangu nilisema nisikuchoshe. Nikuache upumzike, uwe imara zaidi. Basi pumzika na hili pia;

“We cannot be sure of having something to live for unless we are willing to die for it”  (Hatuwezi kuwa na uhakika wa kulipambania jambo mpaka kwanza tuwe tayari kufa kwaajili ya jambo hilo) – Ernesto ‘Che’ Guevara.

Wewe umetuonyesha hilo kwa vitendo na ndio maana upo hospitali Nairobi. Sisi sote twapaswa kuwa Tundu Lissu.

Pole sana Komredi, Mola akupe afya njema.

 

Ridhiwani Kikwete afurahia uzima wa Lissu, aandika haya
LIVE BREAKING: Rais Magufuli apokea ripoti mazungumzo ya Serikali na Barrick