Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Morogoro – MORUWASA imetangaza dau la hadi Shilingi laki tano za papo hapo kama zawadi kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa wezi wa miundombinu ya maji huku ikitoa wito kwa wamiliki wa nyumba kuimalisha ulinzi wa Dira za maji.
Hatua hiyo, inatokana na uwepo wa baadhi ya watu wanaiba dira za maji (Mita) pamoja na maunganisho yake kwa kuuza chuma chakavu, na kukwamisha juhudi za Serikaliza kuendelea kuboresha huduma za maji kwa kujenga miundombinu maeneo mbalimbali nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Morogoro – MORUWASA, Lyang’onjo Kiguhe amesema Kwa kipindi cha mwezi Januari pekee 2023 Dira za maji 52 zimeibwa katika maeneo Mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro na kuleta hasara zaidi ya milioni tano.
Kutokana na chamgamoto hiyo, MORUWASA wamekutana na wanunuzi wa chumachakavu Manispaa ya Morogoro, ili kuwapa elimu ya kutambua mali za mamlaka hiyo na kushiriki kuwakamata wezi wa miundombinu ya maji.
Kwa upande wake Mwanasheria wa MORUWASA, Tumain Kimaro anasema yeyote atakayekamatwa kwa kuharibu au kuiba vifaa vya maji na uchepushaji atafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi na anaweza kulipa faini kuanzia laki tano hadi milioni 50 au kifungo cha miaka mitano.
Naye mmoja wa wauza Chuma chakavu mjini Morogoro Juma John, amesema awali walikua hawafahamu madhara ya kununua vitu hovyo lakin kupitia elimu hiyo watakua walinzi huku Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoani Morogoro, Hassan Omary akisema wataendelea kushirikiana wananchi kuwakamata wezi wa miundombinu ya maji.