Jana, Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowasa alipata mapokezi ya kihistoria jijini Arusha, mapokezi ambayo yanatajwa kuvunja rekodi za mikutano yote ya kampeni jijini humo.

Taarifa za uhakika kutoka jijini humo zinaeleza kuwa watu walianza kumiminika katika viwanja vya Sinoni kuanzia majira ya saa tatu asubuhi wakimsubiria Lowassa na viongozi wengine wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa.

Maelfu ya wananchi hao walivumilia hali ya jua na baadae mvua iliyoanza kunyesha wakati mkutano huo ukiendelea, huku kivutio kikubwa kikiwa Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ambaye alipanda rasmi kwa mara ya kwanza kwenye jukwaa la Ukawa kumnadi Lowassa.

OTH_4335

Msafara wa mapokezi ya Lowassa ulikuwa wa historia ya mafuriko ya watu katika kila barabara alizopita huku shughuli zikisimama ili kupisha zoezi hilo la kisiasa.

Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye pamoja na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walipanda jukwaani na kuwataka wananchi kutokubali kurubuniwa na viongozi wa CCM na kuhakikisha wanafanya mabadiliko na kumchagua Edward Lowassa pamoja na wagombea wengine wa Ukawa.

Edward Lowassa akimnadi mgombea ubunge wa Arusha, Godbless Lema

Edward Lowassa akimnadi mgombea ubunge wa Arusha, Godbless Lema

Mzee Kingunge aliyekaribishwa jukwaani na Mbowe alitumia takribani dakika 40 kuwaeleza wananchi kuwa chama chake hicho cha zamani kimeishiwa pumzi baada ya kutawala kwa zaidiya nusu karne na kwamba kimepoteza muelekeo. Hivyo aliwataka wananchi wakitose na kufanya mabadiliko bila woga.

Kadhalika, Mzee Kingunge aliukosoa uongozi wa rais Jakaya Kikwete kwa madai kuwa imeshindwa kukuza uchumi wa nchi kwa kipindi cha miaka 10.

Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akiongea na wananchi

Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akiongea na wananchi

Mzee Kingunge alieleza kuwa wakati serikali ya awamu ya nne inaingia madarakani uchumi ulikuwa unakuwa kwa asilimia 7 na hivi sasa inandoka madarakani uchumi unakuwa kwa takribani asilimia 7, hivyo uchumi umedumaa.

“Hivi sasa ukuaji wa uchumi wetu, upo unakaribiakaribia asilimia 7, maana yake nini… Maana yake kwa miaka kumi hii tulikwama, waingereza wanaita stagnation,” alisema Kingunge.

Naye muasisi wa Chadema, Mzee Mtei alipata nafasi ya kuzungumza na kuwaeleza wananchi hao kuwa wanayo kila sababu ya kufanya mabadiliko na kwamba rais ajaye anapaswa kusimamia misingi ya demokrasia.

Hatimaye, Edward Lowassa alizungumza na wananchi wa jiji hilo waliokuwa wakimshangilia kila wakati na kupuliza mavuvuzela. Na aliwaomba wampigie kura nyingi kwa kuwa amepanga kuwaletea maendeleo kwa kasi kubwa.

Alitaja vipaumbele vya serikali atayoiunda ikiwa ni pamoja na elimu ya ufundi, kilimo, ajira pamoja na afya.

Alisema kuwa serikali yake itahakikisha mazingira bora ya kufundishia kwa walimu ili waweze kufanya kazi kwa moyo. Na pia elimu bora itakayotolewa bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu, bila kuwa na michango.

Aliwaahidi pia wakulima kuwa atahakikisha wanafaidika na kilimo cha kisasa na kwamba wataweza kuuza mazao yao popote na kwa bei inayofaa.

“Nikichaguliwa kuwa rais nitaanzisha makao makuu yote ya wilaya kuwa na hospitali za rufaa. Watakuwa na vifaa vya kisasa utra sounds, X-Rays na kila kitu cha kisasa kitakuwa katika hospitali ya wilaya,” alisema Lowassa.

Lowassa aliwasisitiza wananchi hao kuhakikisha wanampigia kura kwa wingi kwa kuwa kura ndizo zitakazomuingiza ikulu na sio kelele za kushangiliwa pekee. Aliwataka wananchi hao kupiga kura wa wingi akidai kuwa CCM wana historia ya kuiba kura hivyo wakishapiga kura wahakikishe wanazilinda.

Esther Bulaya Ashtakiwa Kwa Jaribio La Kuvamia Kituo Cha Polisi, Alazwa Selo
Robert Lewandowski Achana Tiketi Ya Scotland