Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani wamemuomba Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson kuridhia hoja yao ya kuitaka Serikali kufuta posho za vikao kwa wabunge wote ili fedha hizo zielekezwe katika huduma nyingine za kuwaletea wananchi maendeleo.

Ujumbe huo umetolewa na msemaji wa Kambi hiyo, David Silinde (Chadema) alipokuwa akiwasilisha maoni ya Kambi hiyo kuhusu hotuba ya Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/17.

Silinde ambaye ni Mbunge wa Momba, alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Naibu Spika kuagiza wabunge wote wa wanaosusia vikao vya Bunge na kutoka nje kufanya shughuli ambazo sio za Bunge wasilipwe posho.

Msemaji huyo wa Chadema alikanusha taarifa iliyotolewa na baadhi ya wabunge wa CCM kuwa wapinzani hao husaini mahudhurio ili wachukue posho na kisha kuondoka Bungeni.

“Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti ya Serikali ya 2016/17, napenda kuweka rekodi sawa kuhusu upotoshaji unaofanywa na Wabunge wa CCM kwamba Wabunge wa Upinzani wanaisaini mahudhurio bungeni na kuchukua posho bila kufanya kazi,” alisema Silinde.

“Napenda mkumbuke kwamba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikisisitiza kufutwa kwa posho za vikao kwa maana ya “Sitting allowance”, lakini serikali imekuwa ikipata kigugumizi, hivyo basi Kambi Rasmi inasema kama kweli Serikali ya Rais John Pombe Magufuli inania thabiti ya kubana matumizi ya Serikali basi inoneshe uthabiti huo kwa kuifuta posho ya vikao na fedha hizo zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo hususan kuwapatia Watanzania maji safi na salama,” aliongeza.

Silinde alisema kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza Wabunge wanaoingia Bungeni na kukaa kimya bila kuchangia mijadala hata kwa maandishi wafuatiliwe na wakatwe kwenye mishahara yao kwa kutofanya kazi.

Mbowe afungiwa Hotelini, akamatwa na kugomea masharti ya polisi
Ole Medeye aikimbia Chadema, amtetea Naibu Spika