Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amezitaka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC, zishirikiane kutumia rasilimali zilizopo kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Jumuiya hiyo.

Dkt. Tulia ameyasema hayo wakati akitoa neno la shukran kwa niaba ya Maspika wenzake baada ya Rais wa Jamhuri ya Seychelles Mhe. Wavel Ramkalawan kufungua Mkutano wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Kibunge la nchi za SADC (SADC-PF) unaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Eden Blue uliopo Mahe nchini Seychelles leo tarehe 27 Mei, 2023.

Akitoa mfano wa ushirikiano huo, Dkt. Tulia amesema “nchi wanachama wa SADC wanaweza kutumia mafanikio yanayopatikana kwenye sekta ya uvuvi nchini Seychelles na vivyo hivyo Tanzania inaweza ikatumika kutatua changamoto za uhaba wa chakula unazozikabili nchi nyingine katika Jumuiya hiyo.”

Aidha, Dkt. Tulia anatarajiwa kuitaarifu Kamati hiyo juu ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 53 wa Jukwaa hilo unaotarajiwa kufanyika tarehe 2 – 8 Julai, 2023 Jijini Arusha, ambapo Bunge la Tanzania ndilo mwenyeji wa Mkutano huo.

Rais Samia ataka uzingatiaji kiapo cha uaminifu, utunzaji siri
Kocha Young Africans asikitika kumkosa Aucho