Wanasayansi wa Marekani wamesema mfumo wa hali ya hewa unaojulikana kama El Nino umeanza katika bahari ya Pasifiki na kuongeza wasiwasi wa ongezeko la joto duniani linatotarajia kufikia kiwango cha nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Celcius.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya mataifa kuanza maandalizi ya kukabiliana na hali mbaya ya hewa ikiwemo vimbunga na mafuriko hasa katika mataifa ya Amerika ya Kusini na Pembe ya Afrika.
Mamlaka ya hali ya hewa ya Marekani – NOAA, kupitia Mwanasayansi wake, Tom Di Liberto imetahadharisha kuwa El Nino huenda ukaufanya mwaka ujao 2024 kuwa mwaka wenye joto zaidi duniani na kuvunja rekodi ya ongezeko la joto duniani tangu mwaka 2016.
Tofauti na mfumo wa hali ya hewa wa La Nina, ambao aghalabu hupunguza viwango vya joto duniani na ambao umeshuhudiwa kwa miaka mitatu iliyopita, kinyume chake El Nino inahusishwa na kupanda kwa viwango vya joto.