Mchezaji wa Simba Abdi Banda, anaedaiwa kufanya kosa la utovu wa nidhamu dhidi ya kocha wa klabu hiyo Jackson Mayanja, ameibuka na kupinga madai hayo kwa kusema hakubaliani na taarifa hizo.

Banda ameibuka na kudai hiyo, baada ya kocha Mayanja kuthibitisha kwamba, mchezaji huyo alionyesha utovu wa nidhamu wakati wa mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Coastal Union, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.

Banda amesema anashangazwa na taarifa hizo kusambazwa kwa makusudi, huku akisisitiza hakuna baya lolote alilolifanya dhidi ya kocha huyo kutoka nchini Uganda, ambaye alipewa jukumu kuwa mkuu wa benchi la ufundi mara baada ya kuondoka kwa Dylan Kerr.

“Unajua watu wakishaona mnaendelea vizuri katika timu yenu hasa kipindi hiki cha kuuwania ubingwa, mambo mengi yanaibuka lakini siwashangai sana kwakuwa ni kawaida yao” alisema Banda

“Pamoja na yote hayo siwezi kuongea sana juu ya tuhuma zangu, labda uwaulize viongozi kwa sababu wao ndiyo wameongea kwamba mimi sina nidhamu” Banda aliongeza kwa kusema kauli hiyo.

Taarifa zilizopo zinadai kwamba, hii leo uongozi wa klabu ya Simba huenda ukafanya mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia suala hilo, pamoja na mambo mengine ya klabu hiyo.

TFF Waendelea Kusisitiza Hili Lisifanyike
Zitto ajiuzulu rasmi, ataka Spika awatumbue wabunge waliokula rushwa