Mabingwa wa soka nchini England Man city wamedhamiria kumuweka sokoni mlinda mlango Joe Hart kwa thamani ya Pauni milioni 5, ili kufanikisha lengo lake la kuondoka jumla klabuni hapo.

Man City wamedhamiria kufanya hivyo, kutokana na hitaji la mlinda mlango huyo kutaka kucheza mara kwa mara, baada ya msimu uliopita kupelekwa kwa mkopo West Ham Utd.

Kwa mujibu wa gazeti la The Times, taarifa zinaeleza kuwa, uongozi wa klabu hiyo ya mjini Manchester tayari umeshakutana na meneja Pep Guardiola kwa lengo la kufahamu mustakabili wa mlinda mlango huyo, na maazimio yaliyofikiwa ni kuhakikisha Hart anaondoka klabuni hapo kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi.

Hart, mwenye umri wa miaka 31, kwa sasa yupo na kikosi cha Man City katika ziara ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi huko nchini Marekani, na ameshacheza michezo yote ya majaribio.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini Marekani vimefanya mahojiano na mlinda mlango huyo wa zamani wa kikosi cha timu ya taifa ya England, na amedhihirisha lengo lake la kutaka kucheza mara kwa mara, huku akisisitiza hitaji la kuondoka klabuni hapo na kwenda mahala pengine.

“Ninahitaji kwenda mahala pengine, nitafurahia kama nitaondoka jumla,  sio kwa mkopo kama ilivyokua misimu miwili iliyopita nilipopelekwa nchini Italia kwenye klabu ya Torino kisha West Ham Utd,” alisema Hart.

“Lengo langu ni kuhitaji mahala ambapo nitatulia na kutimiza mipango  ya kucheza kila mwishoni mwa juma, tena katika kikosi cha kwanza.

“Nina uzoefu wa kutosha. Nimecheza katika kiwango cha juu hadi nimefikia hatua niliopo hivi sasa, haipendezi kuendelea kutolewa kwa mkopo ili hali katika kikosi cha kwanza cha Man city ninajua siwezi kupata nafasi.”

“Nipo tayari kwa mapambano ya kuwania nafasi katika kikosi cha kwanza popote nitakapokwenda, ninajiamini kwa sababu nina umri wa miaka 31 ambao ni mdogo sana, nipo vizuri na nina uhakika nikipata nafasi nitaushangaza ulimwengu.”

Hart hakuitwa kwenye kikosi cha England kilichoshiriki fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwezi uliopita, kufuatia kiwango chake kutomridhisha kocha mkuu wa The Three Lions Gareth Southgate, na badala yake alimchukua mlinda mlango wa Everton Pickford.

Mama azaa mapacha 5, baba anusurika kukimbia familia
Serikali yawabana wachungaji, yataka makanisa kutozwa ushuru