Meneja wa klabu bingwa nchini England Antonio Conte ameanza kupata hofu ya kikosi chake huenda kikashindwa kumaliza katika nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi ya EPL msimu huu, kutokana na ushindani.

Conte amesema maneno hayo na kuchukuliwa kama onyo kwa wachezaji wake ambao mwishoni mwa juma lililopita walishindwa kufurukuta mbele ya wagonga nyundo wa jijini London (West Ham Utd), kwa kufungwa bao moja kwa sifuri.

Kutokana na matokeo hayo, Chelsea wameachwa kwa pengo la alama 14 na Manchester City wanaoongoza msimamo wa ligi ya EPL, licha ya Manchester United, Liverpool na Arsenal kupoteza pointi katika michezo ya mwishoni mwa juma lililopita.

Chelsea inabaki katika nafasi ya tatu, lakini Conte amesisitiza kipaumbele chao ni kuhakikisha wanafuzu kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao, baada ya kukata tamaa ya kutetea ubingwa.

“Kuna tatizo kwenye hii ligi. Kuna timu sita za juu na kuna nafasi nne tu kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa na nafasi mbili kwa ajili ya Ligi ya Europa,” aliwaambia waandishi.

“Tuna malengo, pia kama Manchester City wana pointi nyingi juu yetu, tuna lengo moja ambalo ni kujitahidi kutinga nne bora na kucheza Ligi ya Mabingwa. Bila kusahau, miaka miwili iliyopita Chelsea walikosa kushiriki, msimu uliopita hatukucheza michuano ya Ulaya.

“Shabaha yetu ni kucheza ligi. Narudia, tuna malengo yetu na ni lazima tupate nafasi katika nne bora kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa.

“Usisahau kwamba msimu uliopita Arsenal na Manchester United walikuwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa, kisha United wakatwaa taji la Ligi ya Europa, lakini vinginevyo Manchester United na Arsenal zingekosa. Shabaha hii ni muhimu sana kwangu, kwa wachezaji na kwa kila mmoja. Narudia, si kazi rahisi kutinga nne bora.”

Chelsea wataikabili Huddersfield Town kwenye uwanja wa John Smiths kesho Jumanne wakilenga kurudi kwenye njia ya ushindani.

Kilimanjaro Stars fungu la kukosa, yachapwa tena
Okwi awashangaa viongozi Simba SC