Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (OR-TAMISEMI), kupitia kitengo cha uratibu wa Mradi wa Bonde la Mto Msimbazi kinachosimamiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini – TARURA, imeautaarufu umma kuanza kwa zoezi la ubomoaji wa nyumba zilizofidiwa na mradi wa uendelezaji wa bonde la msimbazi.

Taatifa iliyotolewa hii leo Machi 25, 2024 na Mhandisi Humphrey Kanyenye imeeleza kuwa kwa mujibu wa makubaliano ya utekelezaji wa zoezi, waathirika waliokwishapokea malipo yao wanatakiwa kuhamisha mali zao na kupisha eneo la mradi ndani ya wiki 6 baada ya kupokea fedha hizo.

Mhandisi Kanyenye ambaye ni Mratibu wa Miradi ya ushirikiano na Benki ya Dunia TARURA, kupitia tqarifa hiyo ameeleza kuwa, jumla ya waathirika 2155 kati ya waathirika 2329 wamelipwa kiasi cha shilingi 52,612,072,623.15.

Ofisi ya uratibu kwa kushirikiana na ofisi ya Wakurugenzi wa jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Kinondoni, inatarajia kuanza zoezi la ubomoaji wa nyumba zilizofidiwa April 12, 2024.

Hata hivyo, zoezi hili litawahusu wale ambao wamefikisha wiki 6 toka wapokee malipo yao ambapo awamu ya pili ya fidia ya waathirika 446, malipo yao yako tayari na mthamini Mkuu wa Serikali atasaini Machi 26, tayari kwa malipo.

Taarifa ya Mhandisi Kanyenye pia imeeleza kuwa Wananchi wenye maswali au wanaohitaji maelezo zaidi kuhusu zoezi la ubomoaji wawasiliane na ofisi ya mratibu mradi kupitia nambari ya what’sapp 0738 35 38 54 kwa kutuma ujumbe au kupiga simu kwa nambari 0738 35 38 55.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 26, 2024
Jumaa: Msijitangaze, tangazeni utekelezaji ilani ya CCM