Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) limesema kuwa linamtafuta mkali wa RnB, Ben Pol kwa lengo la kumhoji kuhusu picha zake zinazoonekana mtandaoni zikimuonesha akiwa hajavalia chochote, huku akiwa amefungwa kama mateka.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Godfrey Mngereza amesema kuwa tangu walipoziona picha hizo walianza kufanya juhudi za kumpata msanii huyo ili wafahamu kama ana tatizo la akili au tatizo la kimaadili.
“Sisi kama BASATA tumeona hizo picha mtandaoni, siyo kitu kizuri, kwanza hakiendani na tamaduni zetu. Kwahiyo sisi tunamtafuta Ben Pol halafu tumsikilize, atueleze zile picha ilikuwaje mpaka zikasambaa mitandaoni. Tukiongea naye tunaweza kutoa kauli yoyote na kulaani matukio ya namna hiyo,” Mngereza anakaririwa na mtandao wa Bongo5.
Aliongeza kuwa Baraza linaungana na baadhi ya wasanii na wananchi waliolaani picha hizo, na kwamba wao pia hawawezi kukaa kimya kuhusu tukio hilo.
Ben Pol alipost kwenye Instagram picha mbili, moja inamuonesha akiwa mtupu (bila kuonesha sehemu za siri), akiwa amefungwa kama mateka akionekana sehemu ya mgogoni, na ya pili iliyomuonesha uso na kifua kilichoandikwa namba 3.
Baada ya siku moja ya gumzo mtandaoni, Ben Pol aliweka kipande cha wimbo ambao ndani anasikika yeye akiwa na rapa Darassa na kuandika, “usi-judge kitabu kama hujakisoma ndani.”