Shirikisho la soka nchini Libya (LFF), limetangaza kumtimua kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo Javier Clemente, baada ya kuambulia kisago cha kufungwa mabao manne kwa sifuri katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 dhidi ya timu ya taifa ya Jamuhuri Ya Kidemokrasia Ya Kongo.

Mapema hii leo shirikisho la soka la nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika lilitoa taarifa ya kumtimua kocha huyo kutoka nchini Hispania kwa kuamini kichapo walichokipokea katika mchezo huo wa kundi A ambao ulichezwa mjini Kinshasa siku ya jumamosi ni sawa na dharau.

Hata hivyo bado kuna majadiliano baina ya maafisa wa shirikisho la soka nchini Libya kuhusu kuondoka kwa Clemente, ambapo kati yao wamependekeza aachiwe timu hadi mwishoni mwa mwaka huu na wengine wanataka aondoke mara moja.

Maafisa waliopendekeza kocha huyo kubaki hadi mwishoni mwa mwaka huu, wanaamini uwepo wa Clemente huenda ukasaidia katika michezo miwili ya kundi A ambayo Libya watacheza dhidi ya Guinea na Tunisia.

Clemente mwenye umri wa miaka 66, amewahi kuinoa timu ya taifa ya Cameroon kwa upande wa Afrika, na kwa Ulaya amewahi kuwa kocha mkuu wa timu za taifa za Hispania pamoja na Serbia.

Video: Maelezo ya mwalimu aliyempiga mwanafunzi Mbeya
Joe Hart: Torino Ni Mahala Sahihi Kwa Mchezaji Kama Mimi