Gwiji wa soka nchini Amri Kiemba ameikingia kifua klabu ya Young Africans, kufuatia matokeo ya mchezo dhidi ya KMC FC, ambayo yalipokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa soka.

Young Africans ililazimisha sare ya bao moja kwa moja, baada ya kutanguliwa kufungwa na KMC FC katika kipindi cha kwanza kabla ya kusawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Yacoub Songne.

Matokeo hayo yameendelea kuiweka Young Africans kwenye wakati mgumu wa kusaka taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, ambalo kwa misimu mitatu mfululizo linamilikwa na watani zao wa jadi Simba SC.

Kiemba amesema haoni kama Young Africans walifanya vibaya kwenye mchezo huo, kwani anaamini wachezaji wao walionesha kiwango cha kupambana kama walivyoandaliwa na Kaimu Kocha Mkuu Juma Mwambusi.

“Mimi sioni kama Young Africans imefanya vibaya, timu yao walivyoitengeneza bado wamefanikiwa! Wanatakiwa kuendelea kukazia hapo, ili kuona msimu ujao wataendelea hadi wapi.”

“Shida ya Young Africans sasa hivi ni kutaka kujilinganisha na Simba SC, hawajipimi kwa mafanikio na kile ambacho wamekifanya mpaka sasa hivi kimewalipa kwa kiasi gani.”

“Hawakuwa na wachezaji, wamesajili wachezaji, tangu wamesajili hadi sasa wamefikia wapi wao wanaangalia Simba imefika wapi. Wakati Simba inahangaika kutengeneza hii timu Young Africans ilikuwa inachukua mataji.”

“Young Africans inatakiwa kufuata mchakato haitatokea wanashinda ubingwa tu, bila kujipanga.”

“Kama wana malengo ya msimu ujao waendelee kukazia hapohapo, warekebishe kwenye mapungufu na kujua wanakujaje. Msimu huu wamekusanya wachezaji na wameonesha ushindani kwenye ligi.”

“Hawana haja ya kuaiangalia Simba kwa sababu wenzao walianza safari yao miaka minne iliyopita wao ndio wameanza mwaka huu. Wanawezaje kuwa sawa?  Simba tayari imeshatembea umbali mrefu kwa hiyo hawawezi kuwa sawa , lakini wanaweza kuwafukuza wakawakuta njiani na wakawapita.”Amesema Kiemba ambaye aliwahi kuzitumikia Simba SC na Young Africans kwa nyakati tofauti.

Serikali yawapatia ufumbuzi wakulima wa Ufuta, Korosho
Ujenzi bomba la mafuta fursa kwa Tanzania