Kocha mkuu wa Kitayosce, Henry Mkanwa amesema hatakurupuka kwenye usajili wa wachezaji isipokuwa atakuwa makini kutafuta watu wa kazi watakaoiwezesha kukaa Ligi Kuu muda mrefu, huku akichekelea rekodi yake.

Mkanwa alikabidhiwa timu hiyo mzunguko wa pili akichukua mikoba zilizoiwe ya Ahmed Soliman raia wa Misri, ambapo amefanikiwa kuipandisha daraja na msimu ujao itakiwasha katika Ligi Kuu Bara.

Kocha huyo anafikisha timu nne alizozipeleka Ligi Kuu akianza na Polisi Dodoma (sasa Dodoma Jiji), Polisi Moro (kisha Polisi Mara na sasa ni Biashara United) na sasa ameipandisha Kitayosce.

Kocha huyo amesema tayari wamevunja kambi wakiendelea na mapumziko huku akiwa tayari amekabidhi ripoti kwa viongozi ya mastaa anaowataka msimu ujao.

Amesema katika usajili hatakurupuka, bali atakuwa makini kuangalia nani awe naye msimu ujao na kwamba, anachotaka Kitayosce idumu katika Ligi Kuu na siyo msimu mmoja na kurudi Championship.

“Bahati nzuri nimecheza soka la ushindani kwa miaka 14. Wachezaji wote hapa Tanzania nawajua, hivyo siwezi kutenga muda kumfuatilia mmoja mmoja muda ukifika nitajua nani niende naye.

“Najivunia kuendeleza heshima na rekodi yangu kupandisha timu Ligi Kuu, lazima makocha wazawa tupewe heshima siyo kila muda wanakumbatiwa wale wa kigeni,” amesema Mkanwa aliyewahi kuzichezea Reli FC na Polisi Morogoro hadi kutundika daruga mwaka 2004.

Ameongeza kuwa atatumia vyema uwezo na uzoefu alionao kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri Ligi Kuu msimu ujao 2023/24.

Mashujaa FC yatamba safari ya Mwanza
DRC yawachomea utambi M23, RDF Mahakama ya uhalifu