Serikali nchini imezifungia maabara 13 ambazo sawa na asilimia 21 ya maabara 61 zilozokaguliwa, na kutoa onyo kwa Maabara nyingine 48 ambazo hazijakidhi viwango vya utoaji huduma za upimaji kwa jamii.

Msajili wa Bodi ya Maabara Binafsi kutoka Wizara ya Afya Dominic Fwiling’afu, ameyasema hayo hii leo wakati wa ziara ya ukaguzi wa hali ya utoaji huduma za upimaji katika maabara zilizopo Jijini Dodoma.

Amesema Bodi ya Maabara Binafsi inaendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kukagua maabara Binafsi zilizopo nchini, na kwamba hawatosita kuchukua hatua kwa maabara zilizo na mapungufu ili kuhakikisha zinatoa huduma bora kwa wananchi kulingana na mwongozo uliotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya.

“Kati ya maabara 61 tulizozikagua, maabara 8 ambazo ni sawa na asilimia 20 zipo ndani ya vituo vya kutolea huduma kama vile zahanati na maabara zinazojitegemea ni 5 zilizo sawa na asilimia 24, na utaratibu wa ukaguzi unafanyika nchi nzima kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi” Amefafanua Fwiling’afu.

Amesema zoezi hilo limeanza Jijini Dodoma likiwa na lengo la kukagua jumla ya maabara 106, ili kujiridhisha endapo utoaji huduma upo sahihi kwa wananchi, ikiwemo kukagua endapo Wataalamu waliopo katika Maabara hizo wanakidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria.

Fwiling’afu amesema licha ya kukagua ili kujiridhisha na ubora wa huduma zinazotolewa na Maabara hizo, pia Bodi hiyo inajukumu la kuangalia ulipaji wa tozo mbalimbali uliowekwa kwa mujibu wa Sheria na kujiridhisha iwapo maabara hizo zimetimiza masharti wakati wa kuanzishwaji kwake.

“Bodi pia itakua na jukumu la kuangalia kama maabara zote zinafuata miongozo kwa mujibu wa sheria na kuangalia utendaji wake wa utoaji huduma katika Maabara kama ni sahihi na salama na tutaangalia sheria inasemaje kwa walio nje ya vigezo,” amesisitiza.

Hata hivyo Fwiling’afu amesema pamoja na zoezi hilo pia bodi itaendelea kutoa ushauri kwa wamiliki na wataalamu wa maabara ili kutoa huduma bora na kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanapata huduma kwenye maabara zilizosajiliwa kisheria.

Awali, Mkaguzi kutoka Bodi ya Maabara Binafsi Wizara ya Afya Bi. Mayasa Rico, amesema wamezifungia maabara hizo kutokana na kukosekana kwa wataalamu wa maabara wenye sifa, kuendesha maabara hizo bila ya kuwa na vibali, kutokuwa na miongozo na kanuni ya Bodi, miundombinu kutokidhi viwango, kutoa huduma za matibabu na kutoa huduma baadhi ya huduma bila kibali.

“Kuna baadhi ya sehemu wanapima vipimo visivyoruhusiwa bila ya vibali hata wanatoa huduma za matibabu ndani ya Maabara, hizi ni moja ya baadhi ya sababu zinazopelekea kufungwa kwa hizo maabara maana ni lazima kufuata utaratibu,” amesema Bi. Rico.

Kwa upande wake Mkaguzi kutoka Bodi ya maabara Binafsi Wizara ya Afya Edinanth Ģareba, amesema ni maabara 42 pekee ndizo zimesajiliwa na kutambulika kisheria kati ya Maabara 61 zilizokaguliwa, ambazo ni sawa na asilimia 69, huku akisisitiza shughuli zote za maabara kufanywa na mtaalamu wa Maabara pekee.

Video: Gari la CocaCola lapata ajali mbaya
Tanzania yaichakaza Sudan yatinga fainali CECAFA