Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imetoa ufafanuzi kufuatia madai ya Mwanafunzi Josephat John aliyekuwa anasoma kidato cha nne shule ya Sekondari Kom iliyopo kwenye Manispaa ya Shinyanga a ambaye alizua taharuki baada ya kujianika juani huku akiwa amevaa mabango yenye ujumbe wa kupinga kuchaguliwa masomo ya biashara (ECA) ambayo anadai hajawahi kusomea kwani yeye amesoma masomo ya Sayansi (PCB).

“Mwanafunzi huyo amepata Div II:21 na masomo ya sayansi anayodai amesomea amepata DCC yenye jumla ya pointi 10, Mwisho wa pointi za wanafunzi waliopangiwa tahasusi hii ni 8 sawa na BCC, hivyo mwanafunzi huyu hajakidhi vigezo vya kuchaguliwa katika tahasusi hii ya PCB kulingana na idadi ya nafasi zilizopo mwaka huu.”

“Hata hivyo Mwanafunzi huyu hajapangiwa tahasusi ya Biashara (ECA) kama anavyodai, bali amepangiwa kusoma Stashahada Maalumu ya Ualimu kwa Masomo ya Physicis na Hesabu katika chuo cha Ualimu Songea ambapo ni miongoni mwa Maeneo aliyochagua katika machaguo ya vyuo alianza na Ufundi, Afya kisha Elimu”.

OR TAMISEMI inaendelea kumtafuta mwanafunzi huyo ili iweze kufahamu nia na shida ambayo amekumbana nayo mpaka kufikia kufanya kitendo hicho.

OR TAMISEMI inaendelea kusisitiza kama kuna mzazi au mlezi yoyote anahitaji ufafanuzi wowote awasiliane na kituo chao cha huduma kwa wateja kwa kupiga simu namba 0735-160201 na 0262-160201 kuandika barua pepe kwenye anwani yetu huduma@tamisemi.go.tz

Serikali yaahidi kuwalinda wamachinga
Tanzania, msumbiji zajadili hali ya usalama