Daraja la Mto Momba linalounganisha mikoa ya Rukwa na Songwe linatarajiwa kufufua fursa za kiuchumi katika mikoa ya magharibi na kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, alipokuwa akikagua ujenzi wa daraja hilo na kuwahakikishia wananchi wa Wilaya ya Sumbawanga kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha daraja hilo linakamilika mwezi Agosti mwakani.

“Toeni ushirikiano unaostahili kwa mkandarasi ili Daraja hili la Momba na madaraja madogo saba yanayojengwa katika barabara ya Kasansa-Kilyamatundu yenye urefu wa Km 210.38 yakamilike kwa wakati”, amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa nia ya Serikali ya kujenga barabara ya Kasansa-Kilyamatundu KM 210.38 na Stalike-Kilyamatundu-Mloo KM 500 kwa kiwango cha lami ili kuongeza kasi ya uzalishaji na usambazaji wa mazao ya kilimo na mifugo katika Bonde la Mto Rukwa kwenda maeneo mingine ya nchi.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Rukwa Eng. Masuka Mkina amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa watamsimamia kikamilifu mkandarasi anayejenga Daraja la Momba na madaraja madogo saba katika barabara ya Kasansa-Kilyamatundu KM 210.38 ili kazi ujenzi huo ukamilike kwa wakati.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kwela, Ignas Malocha amewataka wananchi watakaopata fursa za ujenzi wa madaraja hayo kuepuka vitendo vya wizi na hujuma kwa wakandarasi.

 

Wasanii wasio na maadili kushughulikiwa
Liverpool yaishushia Maribor kipigo cha mwizi, Spurs, Madrid hakuna mbabe