Imebainika rais wa klabu ya Benfica Luis Filipe Vieira mapema hii leo ameelekea mjini Manchester nchini England.

Taarifa zimedai kuwa, Vieira amewasili mjini humo, kwa lengo la kufanya mazungumzo ya mwisho na viongozi wa Man Utd kwa ajili ya usajili wa mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Ureno Gonçalo Manuel Ganchinho Guedes.

Awali ilielezwa kuwa safari ya rais huyo itamjumuisha wakala wa Guedes (Jorge Mendes), ili kuharakisha dili hilo kabla ya dirisha dogo halijafungwa siku nane zijazo.

Vieira anatarajia kufanya biashara ya kumuuza Guedes kwa ada ya uhamisho wa Pauni milioni 30.

Hata hivyo tayari kuna uwezekano wa uwepo wa ushindani katika usajili wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20, kufuatia mipango inayoendelea kusukwa na klabu za nchini Ufaransa AS Monaco pamoja na PSG.

Klabu hizo zimekua katika mawindo ya kumsajili Guedes, na zimekua kimya kwa muda mrefu, lakini inahisiwa huenda walikua wanasubiri kusikia thamani ya mchezaji huyo ambayo tayari imeshawekwa wazi.

Alipoulizwa meneja wa Benfica Rui Vitoria kuhusu uwezekano wa kuondoka kwa mshambuliaji huyo kinda alisema: “Sina uthibitisho wowote kama Gonçalo ataondoka katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

“Rais anajua nini anachokofanya, kuhusu suala mchezaji huyo na wachezaji wengine.”

Man Utd wamedhamiria kumsajili Guedes, ili kuziba pengo lililoachwa wazi na mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Uholanzi Memphis Depay, ambaye mwishoni mwa juma lililopita alijiunga na klabu ya Olympic Marseille ya Ufaransa.

DJ D Ommy azindua App yake ya Simu yenye mzigo mnono, ‘WashaWasha’
Kevin Veltman Akiri Kuitamani West Ham Utd