Imefahamika Rasmi Klabu ya Mtibwa Sugar imemwajiri Kocha Mzawa Habibu Kondo kuwa kocha mkuu wa timu hiyo na anaanza majukumu yake leo Jumanne (Julai 18).

Kondo amechukua nafasi ya Kocha Salum Mayanga ambaye Mtibwa Sugar aliachana naye msimu uliopita kutokana na mwenendo mbovu wa timu yao, huku mechi tatu za mwisho zilizokuwa zimebaki zikisimamiwa na Kocha wa Timu ya Vijana Awadh Juma.

Habari kutoka ndani ya timu hiyo, Kondo ambaye aliwahi kuzifundisha Mbeya Kwanza na KMC FC atapewa majukumu yote kama kocha ikiwemo kufanya usajili wa wachezaji ili kuboresha kikosi ili kiwe chenye ushindani.

Hadi sasa, inatajwa Mtibwa Sugar imemalizana na wachezaji Kelvin Sabato na Kelvin Nashoni huku ikidaiwa kuwa na mpango wa kusajili wachezaji 10, kambi ya timu hiyo nayo ikitarajiwa kuanza rasmi juma hili huko Manungu.

Mmoja wa kiongozi wa Mtibwa Sugar amethibitisha kuajiriwa kwa Kondo.

“Walikuwepo makocha wengi waliomba kazi hiyo, hivyo kukawa na vikao vingi kuamua nani atafaa lengo letu lilikuwa ni kupata kocha mzawa, Kondo ndiye amepita kati ya hao wote na atapewa majukumu yote ikiwemo usajili maana anaifahamu Mtibwa Sugar na anafuatilia ligi.

“Tunajua hatujawa na mwenendo mzuri kwenye ligi. Tunaamini atafanya usajili mzuri na faida kwa timu yetu.” amesema kiongozi huyo.

Sergio Busquets atambulishwa Inter Miami
Viongozi 10 waliozibeba nchi zao Afrika – 8. Nnamdi Azikiwe